Twiga Stars 'wajazwa' mamilioni

02Mar 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Twiga Stars 'wajazwa' mamilioni

WACHEZAJI wa Twiga Stars, jana wamepema hamasa ya ushindi kiasi cha Sh. milioni 15 kuelekea mechi ya kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika (AWC) dhidi ya Zimbabwe.

Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu (Twiga Stars).

Timu hizo zinakutana Ijumaa wiki hii kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi, Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini, Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura alisema fedha hizo ni hamasa ya ushindi kwa kila mchezaji.

Kama Twiga watashinda mchezo huo, kila mchezaji atakunja kiasi cha Sh. 300,000 na watapata kiasi kama hicho kama watashinda kwenye mechi ya marudiano.

Naibu waziri huyo alisema iwapo Twiga watashindwa kuwafunga wapinzani, basi fedha hizo hawatapewa, badala yake zitaelekezwa kwenye shughuli zingine.

Aliwataja wadau waliosaidia kupatikana fedha hizo kuwa ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) waliotoa Sh. milioni 10, Kampuni ya Asas Diary (Sh. milioni 2) na mdau mwingine ambaye hakutaka jina lake litangazwe alichangia Sh. milioni 3.

"Nimefurahishwa na nidhamu kubwa mlioonyesha kwenye kambi yenu, naamini mtaifunga Zimbabwe na kusonga mbele," alisema Wambura.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa alimshukuru kiongozi huyo kwa hamasa waliyotoa kwa wachezaji wa Twiga.

Habari Kubwa