Twiga Stars yaanza kuiwinda DR Congo

21Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Twiga Stars yaanza kuiwinda DR Congo

KIKOSI cha wachezaji 27 wa Timu ya Taifa ya Wanawake “Twiga Stars”, kinatarajia kuanza mazoezi rasmi kesho kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kuwania kufuzu Michezo ya Olimpiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) utakaochezwa Aprili 5, mwaka huu, hapa jijini Dar es Salaam.

Timu hiyo inayofundishwa na Bakari Shime pamoja na Edna Lema itasafiri kwenda DRC kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaochezwa Aprili 9, mwaka huu.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Lema aliliambia gazeti hili jana kuwa katika kujiandaa na mechi hiyo, wanatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki ili kujiimarisha zaidi.

"Kambi itaanza leo (jana), lakini mazoezi tutaanza Ijumaa kwa sababu kuna wachezaji ambao wanatoka mikoani, ila muda tulionao utatosha kujipanga kuwakabili DRC," alisema kocha huyo.

Wachezaji walioitwa kujiandaa na mchezo huo ni pamoja na Fatuma Omar, Najiath Abbas (JKT Queens), Gelwa Migomba (Kigoma Sisters), Wema Richard (Mlandizi Queens), Maimuna Hamis (JKT Queens), Enekia Yona (Alliance Queens), Fatuma Issa (Evergreen), Fatuma Khatibu, Happyness Hezron, Stumai Abdallah, Anastazia Antony, Fatuma Bushir, Zena Khamis wote kutoka JKT Queens.

Wengine ni Grace Tony wa Yanga Princess, Mwanahamis Omari (Simba Queens), Donisia Daniel (JKT Queens), Asha Shaban (Kigoma Sisters), Asha Rashid (JKT Queens), Amina Ally (Simba Queens), Irene Elias ( Kigoma Sisters), Fatuma Mustapha (JKT Queens), Dotto Tossy (Simba Queens), Aisha Khamis, Esther Mabanza (Alliance Queens), Tausi Abdallah (Mlandizi Queens), Niwael Khalfan (Marsh Academy na Amina Abdallah kutoka Simba Queens.

Habari Kubwa