Twiga Stars yaanza vema

15Feb 2020
Somoe Ng'itu
Tunisia
Nipashe
Twiga Stars yaanza vema

TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), imeanza vema kampeni ya kuwania ubingwa wa Kombe la UNAF kwa kupata ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Mauritania katika mechi iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Kram hapa jijini Tunis.

Mabao yote ya Twiga Stars yalifungwa katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi, Asma Chouchane wa Tunisia.

Amina Ally alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika mechi hiyo dakika ya saba na kufuatiwa na Oppa Clementi aliyepachika goli la pili dakika ya 15 na Kadosho Shekigenda akifunga la tatu dakika ya 22 ya mchezo huo ulioanza saa 5:00 asubuhi ya hapa sawa na saa 7:00 mchana ya Tunisia.

Bao la nne katika mechi hiyo lilifungwa na Enekia Kasonga huku mshambuliaji mzoefu wa timu hiyo, Mwanahamisi Omary ' Gaucho' akifunga bao la tano la sita huku akaunti ya magoli ikifungwa rasmi na Kadosho dakika ya 44.

Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shime alisema baada ya kumalizika kwa mechi hiyo kuwa mchezo ulianza kwa kasi lakini baada ya kuwasoma, waliweza kumiliki mchezo na kupata mabao yaliyowapa ushindi.

Hata hivyo, Shime alisema wapinzani wao walibadilika katika kipindi cha pili na hivyo timu yake ililazimika kupambana ili kulinda ushindi wao.

"Hata hivyo, tumepoteza nafasi nyingi za mabao katika kipindi cha kwanza na cha pili, ila tulivyowafahamu tukajua wapi tunapaswa kupita na kuwazuia, ushindi huu umetusaidia kujiimarisha kuelekea mechi yetu ya pili," alisema Shime.

Twiga Stars itashuka tena dimbani kesho kuvaana na Algeria wakati wenyeji Tunisia watawakaribisha Mauritania.

Habari Kubwa