Twiga Stars yazitaka 3 za Mauritania leo

14Feb 2020
Somoe Ng'itu
Tunisia
Nipashe
Twiga Stars yazitaka 3 za Mauritania leo

TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), inatarajia kuvaana na Mauritania katika mechi ya kwanza ya kuwania ubingwa wa UNAF itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Kram ulioko jijini Tunis nchini hapa.

Mechi hiyo ya kwanza ya mashindano hayo yanayoshirikisha nchi tano imepangwa kuchezwa kuanzia saa 11:00 kwa saa za hapa sawa na saa 7: 00 mchana kwa saa za Afrika Mashariki.

Akizungumza na Nipashe jijini hapa, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shime alisema wachezaji wake wote wako salama na wako tayari kuanza kuwania ubingwa wa michuano hiyo.

Shime alisema amewaandaa wachezaji wake kupambana na kuwa watulivu katika mchezo huo ili kuanza vema michuano hiyo na kufikia malengo ya kurejea na kombe.

Alisema anaamini kasi waliyokuwa nayo katika mashindano yaliyopita wataiendeleza na kulitangaza vema jina la Tanzania.

"Kiufundi tuko vizuri na tunaamini tutafanya vema katika mashindano haya, siwajui vizuri wapinzani wetu Mauritania zaidi ya jina lao, lakini kimpira baada ya kuwaona uwanjani kwa dakika 10 nitajua mbinu zaidi za kuwamiliki," alisema Shime.

Nahodha Msaidizi wa Twiga Stars, Amina Ally, aliliambia gazeti hili kikosi chao kiko imara na wamekuja Tunisia kwa kazi moja ya kusaka ushindi katika kila mechi watakayocheza.

Amina alisema wanaamini wana uwezo wa kuibuka mabingwa na kulinda heshima waliyopewa ya kualikuwa kwenye michuano hii.
"Kama ambavyo wametuamini, sisi pia tutapambana kuhakikisha tunaanza vizuri na kujiweka katika nafasi nzuri, ukishinda mechi ya kwanza unajiongezea nguvu kuelekea mechi inayofuata, kila mechi kwetu ni sawa na fainali," Amina alisema.

Mechi nyingine ya mashindano hayo itakayochezwa leo itakuwa ni kati ya wenyeji Tunisia dhidi ya Morocco ambayo itaanza saa 10:15 jioni kwa saa za Tanzania.

Habari Kubwa