Uchaguzi Taswa wasogezwa mbele

25Jan 2023
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Uchaguzi Taswa wasogezwa mbele

BARAZA la Michezo la Taifa Tanzania (BMT) limeusogeza mbele uchaguzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa) uliokuwa ufanyike Januari 28, mwaka huu na badala yake umepangwa kufanyika  Februari 2  kutokana na mwitikio mdogo

 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mkuu wa kitengo cha uhusiano na mawasiliano BMT, Najaha Bakari, alisema  wameamua kuusogeza  mbele uchaguzi huo  baada ya kuona mpaka sasa wamejitokeza waandishi 8 kuchukua fomu hizo.

"Baraza linasikitika kuona mpaka sasa waandishi wa habari za michezo Tanzania wana suasua kuchukua fomu za uongozi ndani ya chama hicho tunasisitiza waje kuchukua fomu ili waonyeshe mfano kwenye vyama vingine, alisema Bakari.

Kaimu huyo alisema waandishi wanapaswa kuchukua fomu kwani lengo ni kuona chama hicho kinasimamia utawala bora.

Alisema sifa ya mgombea anatakiwa awe na cheti cha taaluma ya uandishi wa habari kutoka kwenye chuo kinachotambulika nchini.

Wakati huo huo alitangaza uchaguzi wa Chama cha Tenesi Tanzania( TTA) ambao utafanyika Februari 25 mwaka huu.

Alisema nafasi ambazo zinawaniwa katika chama hicho ni Rais, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Katibu Mkuu Msaidizi pamoja wajumbe.

Alivitaka vyama vyote vimuunge mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuhakikisha vyama vya michezo vinasonga mbele.