Uchaguzi Yanga wasimamishwa

12Jan 2019
Renatha Msungu
Dar es Salaam
Nipashe
Uchaguzi Yanga wasimamishwa

UCHAGUZI mdogo wa Yanga uliotarajiwa kufanyika kesho kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Osterbay jijini Dar es Salaam umesimamishwa, imefahamika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Malangwe Mchungahela, alisema kuwa kamati yake imeamua kuahirisha uchaguzi huo baada ya baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kuweka pingamizi mahakamani.

Mchungahela alisema kuwa kamati yake inafahamu vyema na kuheshimu sheria za nchi, hivyo wameamua kusitisha mchakato wa uchaguzi huo ambao ulikuwa unajaza nafasi za baadhi ya viongozi waliojiuzulu.

“Sisi kama Kamati hatutaki kugongana na mhimili wa mahakama, kwa sababu tumesikia kuna sehemu nyingine wameanza kusikiliza mashauri hivyo tumeamua kusimamisha uchaguzi, hautafanyika tena Jumapili hadi tupate amri ya mahakama, ” alisema Mchungahela.

Aliwataka wanachama wote wa Yanga kuendelea kuwa watulivu ili kusubiri mwongozo mpya utakaotolewa na kamati hiyo.

Habari Kubwa