Ufaransa kuwakutanisha wasanii kuitangaza Afrika

11Sep 2021
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Ufaransa kuwakutanisha wasanii kuitangaza Afrika

UBALOZI wa Ufaransa nchini, umeanzisha programu maalum inayowakutanisha wasanii kutoka nchi mbalimbali Afrika kwa ajili ya kufanya sanaa za maonyesho kuwainua wanawake, pamoja na kutangaza utamaduni wa jamii za kiafrika.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Matiko Mniko (kulia), akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa Uzinduzi wa Tamasha la Kitamaduni linalojumuisha wasanii kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kusini, lengo likiwa ni kudumisha tamaduni za kiafrika. Kushoto ni Mwandishi wa Maigizo, Alain Kamal na katikati ni msanii kutoka Kenya, Mammito Eunice. PICHA: JUMANNE JUMA

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa programu hiyo jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Mniko Matiko, alisema uzinduzi huo ni hatua kubwa itakayowawezesha wasanii wa Tanzania kuitangaza nchi pamoja na kutangaza vipaji vyao kimataifa.

Matiko alisema: “Hii ni hatua kubwa katika kukuza utamaduni wa kiafrika, wasanii wetu watakuwa na nafasi ya kubadilishana mawazo pamoja na maarifa ya wasanii wenzao kutoka mataifa mbalimbali".

Alisema serikali itahakikisha inashirikiana na wasanii kuhakikisha programu hiyo inafanikiwa na kuleta manufaa kwa Taifa na wasanii kwa ujumla.

Matiko alisema kwa kuanza kuitangaza programu hiyo hapa nchini itaanza katika mikoa ya Arusha, baadaye Dar es Salaam kisha kumalizia visiwani Zanzibar.

Naye Mtunzi na Mwandaaji wa maigizo ya programu hiyo kutoka Msumbiji, Alain Martial, akizungumza wakati wa uzinduzi huo alisema dhumuni la kuanzishwa kwa tamasha hilo lililopewa jina la ‘Genesis’ ni kutangaza tamaduni za Afrika, pamoja na mila za mataifa mbalimbal ikiwamo Tanzania, Kenya, Uganda, Msumbiji na visiwa vya Comoro.