Ufaransa, Ubelgiji kutoana jasho Dar

19Mar 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Ufaransa, Ubelgiji kutoana jasho Dar

TIMU nane za nchi zinazozungumza Kifaransa zinatarajiwa kutoana jasho mwishoni mwa wiki ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya umoja wa nchi zinazozungumza lugha hiyo duniani, huku mechi kali ikitarajiwa kuwa kati ya Ufaransa na Ubelgiji, imeelezwa.

Mashindano hayo ambayo yataleta pamoja timu za nchi saba pamoja na timu ya umoja wa walimu wanaofundisha Kifaransa jijini Dar es Salaam (Dafta), yatafanyika katika viwanja vya Jakaya Kikwete (JKM Park), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu michezo mbalimbali itakayofanyika wakati wa maadhimisho hayo, Balozi wa Ubelgiji nchini, Peter Van Acker, alisema kutakuwa na makundi manne ya timu ambazo zitacheza robo fainali, nusu fainali na baadaye fainali ili kupata mshindi.

Alizitaja timu hizo kuwa Kundi la Kwanza litaundwa na Uswisi na Morocco, Kundi la Pili litakuwa ni Canada na Rwanda, Kundi la Tatu ni Congo na Dafta, wakati Kundi la Nne likiwa ni Ufaransa na Ubelgiji.

“Timu zote zimefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuukabili mchezo huo, na kila mmoja anataka kuwa mshindi katika mashindano hayo. Hatuishii kuzungumza lugha ya Kifaransa tu, bali tunafanya michezo mbalimbali kwa ajili ya afya zetu na kutuleta pamoja zaidi,” alisema.

Naye Rais wa Dafta, Patrick Shole, alisema timu ya walimu siku zote imekuwa mshindi kwenye mashindano hayo na mengine, na kwamba katika mchezo wa sasa wamejipanga kutunza rekodi ya ushindi kwenye mashindano hayo.

Habari Kubwa