Uholanzi kutathimini utimamu wa Depay

23Nov 2022
Na Mwandishi Wetu
DOHA
Nipashe
Uholanzi kutathimini utimamu wa Depay

LOUIS van Gaal amesema Uholanzi itatathmini utimamu wa kuwa 'fiti' kwa Memphis Depay baada ya ushindi wao dhidi ya Senegal, juzi kwenye Kombe la Dunia.

 

'Oranje' hao waliadhimisha kurejea kwao kwa fainali za Kombe la Dunia kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika, huku mabao ya dakika za lala salama kutoka kwa Cody Gakpo na Davy Klaassen yakiwapa pointi zote tatu katika Kundi A.

Depay alianza mchezo huo akiwa benchi kutokana na tatizo la misuli ya paja linaloendelea, lakini aliingizwa dakika 28 za mwisho kwenye Uwanja wa Al Thumama na fowadi huyo wa Barcelona atatarajia kucheza dhidi ya Ecuador Ijumaa.

"Tulikubaliana kabla ya mchezo kwamba angecheza takriban nusu saa," alisema Van Gaal kuhusu Depay, ambaye amecheza mechi mbili pekee za LaLiga msimu huu.

"Akiwa na Ecuador, atataka kucheza, lakini lazima nipime kiwango chake baada ya mchezo huu. Sikuwahi kufikiria kwamba tutapoteza na kwa kuingia kwa Depay, nilitaka kupata nafasi nyingi za kufunga. Ni mchezaji anayeweza kuleta tofauti."

Van Gaal alisimamia ushindi wake wa 38 akiwa kocha wa Uholanzi, akiweka rekodi kwa kushinda mechi nyingi zaidi kuliko kocha yeyote aliyekiongoza kikosi hicho.

Pia alisifia kiwango cha Gakpo na kipa Andries Noppert, ambaye alifunga bao lake la kwanza kwenye mechi yake ya kwanza ya kimataifa.

 “Gakpo alikuwa na maamuzi, nilimuacha ndani kwa sababu anajua kufunga mabao na ni mwepesi sana,” aliongeza.

"Senegal walikuwa na nafasi tatu, lakini tuna kipa ambaye anajua mambo yake kati ya nguzo.

"Hatukucheza vizuri sana, mara nyingi sana tuliwapa mpira na nafasi ya kufunga.”