Ulimwengu: Mipango ya kwenda Ulaya iko vizuri

08Jan 2017
Mahmoud Zubeiry
Nipashe Jumapili
Ulimwengu: Mipango ya kwenda Ulaya iko vizuri

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu amesema kwamba mpango wake wa kuhamia Ulaya unaendelea vizuri na hivi karibuni atatangaza klabu yake mpya.

Akizungumza na Nipashe jana, Ulimwengu alisema mazungumzo na klabu anayotaka kuhamia yamefikia pazuri na muda si mrefu wanaweza kumalizana.

“Tumefikia pazuri, lakini bado kwa sasa siwezi kusema chochote, kwa sababu bado hatujafikia maafikiano. Tuendelee kuvuta subira hadi mambo yatimie kabisa ndiyo tuweke wazi,”alisema Ulimwengu.

Ulimwengu yupo nchini tangu Novemba mwaka jana baada ya kuhitimisha miaka yake mitano ya kuitumikia klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na sasa anashughulikia mipango ya kuhamia Ulaya.

Na kwa kipindi chote hicho amekuwa akifanya mazoezi makali ya kukimbia mchangani ufukweni, gym na kucheza mpira na timu yake mtaani ili kujiweka fiti wakati akisubiri kusaini timu nyingine.

Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya Athletic FC ya Sweden na kucheza huko hadi 2011 alipochukuliwa na timu ya vijana ya TP Mazembe.

Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza mkataba wake.

Ulimwengu anajivunia kushinda mataji makubwa akiwa na Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.

Habari Kubwa