URA yataja siri kipigoYanga, Simba

12Jan 2018
Nipashe
URA yataja siri kipigoYanga, Simba

WAKATI kesho timu ya URA ikitarajia kushuka dimbani kuivaa Azam FC kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi, kocha wa timu hiyo, Nkata Paul, ametoa siri ya kuibuka na ushindi dhidi ya timu vigogo za Tanzania Bara, Simba na Yanga.

kocha wa timu hiyo, Nkata Paul.

Aidha, amesema alichokifuata Zanzibar ni ubingwa na kikosi chake hakiihofii timu yoyote kwenye michuano hiyo kwa sasa baada ya kuzishuhudia zote zikicheza kwenye michuano hiyo.

URA itakutana na Azam FC kesho katika mechi ya fainali ya michuano hiyo, ikiwa ni baada ya kuitoa Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-4 kwenye mechi ya nusu fainali juzi kufuatia dakika 90 kumalizika timu hizo zikitoka sare tasa, wakati ‘Wanalambalamba’ hao wenyewe wakiitoa Singida United kwa bao 1-0.

Akizungumza na Nipashe juzi, Paul alisema, kwa hatua waliyofikia anaamini watatwaa ubingwa wa michuano hiyo na kwamba haoni sababu ya kushindwa kufanya hivyo kutokana na kikosi chake kuzidi kuimarika kila baada ya mechi.

Alisema siri kubwa ya kikosi chake kuibuka na ushindi dhidi ya Simba na kisha kuichapa Yanga juzi, ni wachezaji wake kucheza kwa ushirikiano katika idara zote.

“Nashukuru wachezaji wangu wamekuwa wakifuata maelekezo, ninayowapa, kikubwa ni kwamba tunacheza kwa umoja kuanzia nyuma hadi safu ya ushambuliaji.

“Tumefika fainali sasa sioni sababu ya kuukosa ubingwa, kwa kuwa timu zote tunazifahamu na zaidi wachezaji wangu wamezidi kujiamini, hivyo sina wasiwasi wa kutwaa ubingwa,”alisema.

Paul alisema atatumia siku mbili (jana na leo) kurekebisha kasoro zilizojitokeza juzi kabla ya kuivaa Azam kwenye mechi ya fainali itakayopigwa kesho katika Uwanja wa Amaan.

Katika mechi hiyo ya juzi, URA iliitoa Yanga kwa penalti 5-4 baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 bila kufungana.

Kipigo hicho cha Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, kama ilivyo kwa Simba, kimekuja ikiwa ni baada ya URA kuwatoa Wekundu wa Msimbazi hao kwa bao 1-0 katika hatua ya robo fainali.

Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alisema walipambana vizuri, lakini siku zote penalti hazina mwenyewe, hivyo wanarejea Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu Bara.

“Penalti huwa hazina mwenyewe, tunawapongeza URA, bahati imewaangukia na wameweza kushinda, hivyo tunarejea Dar es Salaam kujiandaa na Ligi Kuu.

“Kwa ujumla tunashukuru michuano hii imetupa nafasi ya kuchezesha wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi, hivyo tunarejea tukiwa tunajua wapi pakwenda kufanyia kazi,” alisema.

Wafungaji wa penalti za Yanga katika mchezo huo ambao Obrey Chirwa alikosa tuta lake, walikuwa ni Papy Tshishimbi, Hassan Kessy,  Raphael Daudi na Gadiel Michael

Penalti za URA zilifungwa na Kalama Deboss,  Kibumba Enock, Kagimu Shafik,  Kulaba Jimmy na Majwega Brian.  

Habari Kubwa