Urikhob aongeza makali Yanga

17Jul 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Urikhob aongeza makali Yanga

WAKATI mshambuliaji mpya wa kimataifa wa Yanga, Sadney Urikhob, kutoka Namibia amewasili nchini jana kuanza kuitumikia timu yake mpya, uongozi wa mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara, umesema maandalizi ya 'Siku ya Mwananchi’ yako katika hatua za mwisho.

Sadney Urikhob.

Urikhob alipokelewa na viongozi wa klabu hiyo na tayari ameshaelekea mkoani Morogoro kujiunga na wachezaji wenzake kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema kuwa kambi yao inaendelea vema na wanaamini malengo waliyonayo ya kufanya vema katika Ligi Kuu na michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika yatatimia.

“Timu yetu inaendelea vema na mazoezi huko Morogoro, wanafanya vema na wamejiandaa kukabiliana na ushindani, wanafahamu changamoto pia zitakuwa nyingi,” alisema Mwakalebela.

Alisema kuwa Siku ya Mwananchi ambayo itamalizika kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), itakuwa na vionjo mbalimbali na kuwataka mashabiki wa klabu yao wajitokeze kuona wachezaji wao wapya waliosajiliwa.