Usaili wagombea Yanga wakamilika

07Dec 2018
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Usaili wagombea Yanga wakamilika

MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ally Mchungahela, amesema licha ya wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kutohudhuria usaili wa wagombea uongozi katika klabu hiyo, mchakato huo umekwenda vizuri.

Mchakato huo wa usaili ulifanyika jana kama ilivyopangwa tayari kwa ajili ya uchaguzi utakaofanyika Januari 13 mwakani.

Kauli ya kutohudhuria usaili kama walivyotangiwa na Kamati ya TFF, ulithibitishwa na kauli iliyotolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Samuel Lukumay.

“Alikuja mjumbe wao mmoja, lakini alitoudhuru mapema na kuondoka, sisi tunaendelea na taratibu nyingine kama kawaida kwa mujibu wa kalenda tuliyoipanga,” alisema Mchungahela.

Alisema kuwa zoezi hilo lilianza jana majira ya saa 4:30 asubuhi na wanatarajia kukamilisha mchakato huo leo.

“Tuliwapa taarifa kwa barua, tukiwakaribisha kushiriki nasi kwenye zoezi hili, lakini hakuna aliyekuja zaidi ya huyo mmoja naye hakukaa akatoa udhuru, niseme tu sisi tunaendelea na zoezi letu kama tulivyopanga na uchaguzi utafanyika kwa tarehe iliyopangwa,” alisema Mchungahela.

Naye Lukumay alisema hawawezi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi huo kwa kuwa kamati ya TFF haikuwashirikisha tangu mwanzo.

“Nimechaguliwa na klabu kukaimu nafasi ya uenyekiti, nasimamia kanuni za klabu yangu, hatuwezi kushiriki kwenye mchakato ambao hatukushirikishwa hapo awali, wanawafanyia usaili wagombea wao (Kamati ya uchaguzi ya TFF) wanafahamu vipi kama hao wagombea ni wanachama hai wa Yanga,” alisema Lukumay.

Uchaguzi wa Yanga unafanyika kwa kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF baada ya klabu hiyo kukataa kutii maagizo na mwongozo waliopewa na shirikisho hilo pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Habari Kubwa