Usajili Kili Marathon wakaribia kuhitimishwa

11Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Tanga
Nipashe
Usajili Kili Marathon wakaribia kuhitimishwa

USAJILI wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2019, umeingia katika wiki ya mwisho huku zikiwa zimebaki takriban wiki tatu kabla kinyang'anyiro hicho kufanyika mjini hapa.

Katika taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na waandaaji wa mbio hizo, imeeleza usajili utabaki kuwa kwa njia ya mtandao na Tigo Pesa tu, hivyo wanaotaka kushiriki mbio hizo watumie muda uliobaki vizuri ili wasikose nafasi kwani hakutakuwa na usajili tena baada ya Jumamosi Februari 16.

Awali tarehe ya mwisho kujisajili ilikuwa Februari 7, mwaka huu lakini waandaaji wakasogeza mbele ili kuwapa washiriki muda zaidi kutokana na maombi mbalimbali.

“Tumebakiwa na takriban wiki moja tu tufunge usajili na kama tulivyotangaza hapo awali, tuliamua kuongeza siku ili kuhakikisha washiriki wengi wanajisajili, ila tunapenda kukumbusha tu kuwa endapo nafasi zitamalizika mapema, tutafunga usajili kabla ya tarehe ya mwisho,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa waandaaji hao, usajili ni kwa njia ya mtandao kupitia  www.kilimanjaromarathon.com na kulipia kwa njia ya kadi (credit card) au kwa njia ya Tigo Pesa kwa kupiga *149*20# na kufuata masharti.

Aidha, washiriki watapata fursa ya kuchukua namba zao za usajili na fulana za kukimbilia Dar es Salaam, Arusha na Moshi.

Kwa Dar es Salaam, mchakato huo utafanyika Mlimani City Februari 23 na 24  kuanzia saa saba mchana hadi saa moja usiku na kwa Arusha utafanyika pale Kibo Palace Februari 25 na 26 kuanzia saa nane mchana hadi saa mbili usiku  na Moshi ni Februari 27 (saa nne hadi saa kumi na moja jioni)  na Februari 28 kuanzia saa nne asubuhi hadi saa mbili usiku.

Kwa mujibu wa waandaaji, usajili wa mbio za kilometa tano utafanyika katika vituo hivyo vya kutolea namba za kukimbia tarehe hizo hizo zilizotajwa.

 “Tunatoa wito kwa wakazi wa Moshi na Arusha watumie nafasi hii kujisajili kwani wengi wanamazoea ya kusubiri hadi dakika za mwisho…safari hii hakuna usajili Moshi kwa hivyo wasisubiri wajisajili sasa,” ilisema taarifa hiyo.

Mbio hizo za 17 tangu kuanzishwa kwa Kilimanjaro Premium Lager Marathon, mwaka huu zitafanyika Machi 3 katika viwanja vya Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi huku wadhamini wa Km. 42 wakiwa ni Kilimanjaro Premium Lager, Tigo- Km. 21, Grand Malt kilometa tano na wadhamini wa meza za maji na washirika wengine ni KK Security, Keys Hotel, Kilimanjaro Water, TPC Sugar, Simba Cement, AAR, Kibo Palace, Barclays Bank, Precision Air na CMC Automobiles. 

Habari Kubwa