Useme nini tena, hii ndiyo Yanga

13Mar 2016
Lasteck Alfred
Kigali, Rwanda
Nipashe Jumapili
Useme nini tena, hii ndiyo Yanga
  • ***Yalitkisha jiji la Kigali kwa ushindi mzuri Ligi ya Mabingwa Afrika.

ILIKUWA kama mechi ya kisasi cha miaka 20 iliyopita, wakati Yanga ilipolinyamazisha Jiji la Kigali, nchini Rwanda kwa kuwafunga APR mabao 2-1 katika mechi kali iliyojaa kila aina ya burudani.

Wachezaji wa Yanga

APR iliiondoa Yanga kwenye mashindano hayo hatua ya awali kwa kuwanyuka mabao 3-0 katika mechi ya kwanza, Kigali kabla ya wanajangwani kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Slaam.

Lakini jana, haikuwa Yanga ile iliyopoteza mbele ya APR baada ya kuonyesha soka la kuvutia na kuzima kelele na ngebe za mashabiki wa timu hiyo ya jeshi.

Matokeo hayo ni mazuri kwa Yanga kabla ya mchezo wa marudiano, kwani sasa ili isonge mbele itahitaji sare ya aina yoyote.

Kama itafanikiwa kuvuka kikwazo hicho, basi mabingwa hao wa Tanzania Bara watakumbana na miamba ya soka Misri, Al Ahly.

Katika mchezo huo, Yanga ilitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na ingeweza kutoka na ushindi zaidi kama washambuliaji wake wangetumia vizuri nafasi nyingi za kufunga.

Yanga iliandika bao la kwanza kwa kiki ya faulo ya mwendo mrefu iliyopigwa na beki Juma Abdul na kumshinda kipa wa APR, Kwizera Oliver.

Abdul alifumua shuti hilo kali umbali wa zaidi ya mita 30 na kupaa juu ya ukuta wa APR na kwenda moja kwa moja kugusa nyavu katika dakika ya 20.

Thabit Kamusoko aliihakikishia Yanga mwanzo mzuri kabla ya mechi ya marudiano wiki mbili zijazo kwa kufunga bao la pili.

Kamusoko alifunga bao hilo baada kuitendea haki kazi nzuri ya mshambuliaji Donald Ngoma katika dakika ya 74. Kiki ya Kamusoko ndani ya boksi hatari baada ya mabeki wa APR kushindwa kuondoa mbali mpira langoni, ilimshinda kipa wa APR.

Hata hivyo, wakati Yanga wakiamini wanarudi nyumbani na faida ya ushindi wa mabao 2-0, wenyeji wao walizinduka katika muda wa dakika za nyongeza baada ya dakika 90 za kawaida na kufunga la kufutia machozi.

Bao hilo liliwekwa kimiani kirahisi na Patrick Sibomana baada ya kipa wa Yanga, Ally Mustapha kushindwa kuicheza krosi na mpira kumponyoka mikononi mwake na kumkuta mfungaji aliyeusindikiza wavuni mpira kwa shuti dogo.

Baada ya mechi hiyo, wachezaji wa Yanga walikuwa na furaha wakiongozwa na nahodha Haruna Niyonzima aliyekuwa akicheza mechi dhidi ya timu yake ya zamani kabla ya kuhamia Yanga.

Wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam FC walitarajia kushuka dimbani baadaye jana kucheza dhidi ya Bidvest Wits.Kwa habari zaidi za mechi hii, usikose kusoma gazeti la michezo la Lete Raha leo hii.

Yanga:
Ally Mustapha, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Vincent Bossou, Pato Ngonyani, Deus Kaseke, Thabit Kamusoko, Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima.

Habari Kubwa