Utajiri waanza kunukia Yanga

21May 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Utajiri waanza kunukia Yanga
  • Wanachama waambiwa wataendelea kuimiliki klabu licha ya mfumo wa uendeshaji...

MABADILIKO ya mfumo wa uendeshaji yanayotarajiwa kufanyika ndani ya Yanga hivi karibuni yanatajwa yataiongezea thamani klabu hiyo ya jijini Dar es Salaam ambayo inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, imeelezwa.

Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz:PICHA NA MTANDAO

Mchakato rasmi wa mabadiliko ya mfumo huo yalitangazwa kufanyika kuanzia juzi na utasimamiwa na wadhamini wa klabu hiyo, Kampuni ya GSM.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, alisema wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wanatakiwa kutokuwa na hofu ya aina yoyote kwa sababu mabadiliko hayo yatafanyika kwa weledi chini ya Mwanasheria mzoefu, Alex Mgongolwa.

Nugaz alisema viongozi wa klabu hiyo wamedhamiria kuipeleka Yanga kwenye mabadiliko ambayo yatasaidia uendeshaji kuwa wa kisasa.

Alisema kila jambo lina mwanzo na kuanza kwa mchakato huu wa mabadiliko, kutaifanya Yanga kuwa moja ya timu zitakazojiendesha kisasa na kupata mafanikio yaliyokuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu.

"Moja ya azma na sera yake (Mwenyekiti Mshindo Msolla ni kuipeleka Yanga kwenye mabadiliko, kutoka kwenye uendeshaji wa zamani na kwenda kwenye uendeshaji wa kisasa," alisema Nugaz.

Kiongozi huyo aliwataka wanachama wa Yanga kutoa ushirikiano ili mchakato huo ambao ulikwama mara kadhaa miaka ya nyuma ukamilike kwa wakati.

"GSM imekaa sawa, imelivalia njuga suala hili kwenda kwenye mabadiliko, hamu yetu wana Yanga, azma yetu wana Yanga ni kumpa ushirikiano mwenyekiti, kikubwa zaidi ni uzoefu aliokuwa nao huyu mshauri kwa kuongoza timu  42 huko Hispania, tukiungana pamoja, tutakwenda kwenye mabadiliko," alisema Nugaz.

Endapo Yanga itafanikiwa kubadili mfumo wao wa uendeshaji, itakuwa imewafuata watani zao Simba ambayo tayari walishabariki mabadiliko hayo kwenye mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika mwaka 2018.

Katika mchakato huo, Yanga imepanga kutumia kauli isemayo "Twenzetu Kwenye Mabadiliko".

Wakati huo huo Nugaz amesema uongozi umeshajipanga kuwaandalia taratibu za usafiri makocha wake mara mipaka ya anga itakapofunguliwa huko walipo.

Baada ya Ligi Kuu Bara kusimama ili kupisha maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona (COVID 19), Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael na msaidizi wake walikwenda Afrika Kusini kwa ajili ya mapumziko.

Habari Kubwa