Utata tuta la Chirwa  lililoing'oa Yanga 

12Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Utata tuta la Chirwa  lililoing'oa Yanga 
  • ***Waamuzi wastaafu waelezea sheria ya penalti ilivyopindishwa...

WAKATI mashabiki wa Yanga wakiugulia maumivu ya kutolewa kwa mara nyingine katika hatua ya nusu-fainali ya Kombe la Mapinduzi, huenda wakafarijika baada ya kubainika penalti aliyokosa mshambuliaji wao, Obrey Chirwa, ina utata.

Obrey Chirwa.

Akicheza mechi yake ya kwanza ya michuano hiyo mwaka huu, Chirwa, mshambuliaji wa kimataifa kutoka Zambia, alikosa penalti ya mwisho ya Yanga katika hatua ya matuta na kuwapa tiketi watoza ushuru wa Uganda kutinga fainali kwa mikwaju 5-4 baada ya timu hizo kutofungana ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar juzi.

Yanga pia iliondoshwa kwa matuta 4-2 dhidi ya Simba katika hatua ya nusu-fainali ya michuano hiyo mwaka jana. Iling'olewa katika hatua hiyo pia kwa penalti 4-3 dhidi ya URA baada ya kutoka sare ya bao moja ndani ya muda wa kawaida, mwaka juzi.  

Wakati Chirwa sasa akiwa gumzo miongoni mwa wapenzi wa soka nchini, waamuzi wabobezi waliozungumza na Nipashe jana, walisema penalti aliyokosa ilipaswa kurudiwa kwa sababu kipa wa URA, Alionzi Nafian, hakuzingatia kikamilifu Sheria Na. 12 ya Soka (Pigo la Penalti). 

Katibu wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambaye pia ni mwamuzi mstaafu, Kenedy

Mapunda, alisema kisheria penalti ya Chirwa ilipaswa kurudiwa kutokana na golikipa huyo kutoka kwenye mstari wa goli kwa hatua mbili mbele kabla ya kupigwa kwa mpira.

"Kosa la kwanza ni kitendo cha golikipa kutoka mbele kabla ya mpira kupigwa, lakini pia mwamuzi alipaswa kuamuru penalti ile kurudiwa kwa mujibu wa kanuni," alisema Mapunda.

Kauli ya Mapunda iliungwa mkono na mwamuzi mstaafu, Omari Abdulkadir, ambaye alisema waamuzi wa mechi ya URA dhidi ya Yanga hawakutenda haki kwenye penalti ya Chirwa.

"Golikipa anaruhusiwa kusogea akiwa kwenye mstari wake kwenda kushoto au kulia lakini haruhusiwi kusogea kwenda mbele," Abdulkadir alisema na kuongeza kuwa: “Sheria inaweka wazi. Kitendo kama kile mwamuzi alitakiwa kutoa uamuzi wa penalti irudiwe kama mpigaji alikosa, lakini kama lingeingia goli, goli lingekubalika.

"Niliuangalia mpira na kitendo kile nilikiona, nilifikiri penalti ingerudiwa... unajua golikipa siyo asikie filimbi ndiyo atoke kwenye mstari wake, hapana hata kama filimbi imepigwa anatakiwa asitoke kwenye mstari wa goli mpaka mpira upigwe."

SHERIA YENYEWEKatika tukio kama la tuta la Chirwa, Sheria Na. 14 ya Soka inasema: "Kama refa ametoa ishara (amepuliza kipenga) pigo la penalti lifanyike na kabla mpira haujapigwa golikipa anaingilia mchezo, refa ataruhusu pigo liendelee.

"Kama mpira utaingia golini, goli litakubaliwa. Kama mpira usipoingia golini, pigo litarudiwa." 

Habari Kubwa