Utoaji namba Kili Marathon 2021 wahamia Arusha

22Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Kilimanjaro
Nipashe
Utoaji namba Kili Marathon 2021 wahamia Arusha

BAADA ya mamia ya wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza katika viwanja vya Mlimani City jana kuchukua namba zao za ushiriki wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2021, zoezi hilo sasa linahamia jijini Arusha Jumanne na Jumatano.

Akizungumza baada ya kufunga zoezi la kuchukua namba jijini Dar es Salaam, mwakilishi wa Kampuni ya Kilimanjaro Marathon Company, Rajon Datoo, alisema zoezi hilo lilikuwa la mafanikio makubwa kwani watu wengi walijitokeza kuchukua namba zao.

“Tumepokea ushirikiano mkubwa kutoka kwa wakazi wa Dar es Salaam ambao wamefanya zoezi hili liende haraka, tunawaomba waliojisajili mbio ndefu za Kilimanjaro Premium Lager (kilomita 42), mbio za nusu marathon (kilomita 21) za Tigo na zile za kujifurahisha za kilomita tano za Grant Malt wafike Kibo Palace Hotel Jumanne Februari 23 na Februari 24 kuanzia saa nane mchana hadi saa moja usiku,’ alisema na kuongeza kuwa washiriki wanaombwa kukumbuka kwenda na vitambulisho na ujumbe wa uthibitisho wa malipo.

Alisema baada ya Arusha zoezi hilo litahamia Moshi kuanzia Februari 25 saa sita mchana hadi saa kumi na moja jioni), Februari 26 (saa nne asubuhi hadi saa mbili usiku) na Februari 27 (saa tatu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni).

Kwa mujibu wa waandaaji wa mbio hizo, zoezi la uandikishaji kwa washiriki katika mbio za Km 42 na Km 5 bado linaendelea katika vituo vya kutolea namba.

Habari Kubwa