Uwanja mpya Dodoma kukamilika 2021

16Mar 2019
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Uwanja mpya Dodoma kukamilika 2021

UWANJA mpya wa soka unaotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni mkoani Dodoma, utachukua miaka miwili na nusu mpaka kukamilika kwake imefahamika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini, Injinia Patrick Mfugale, alisema ndani ya muda huo uwanja huo utakuwa umekamilika.

Alisema uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuchukua watu kati ya 85,000 mpaka 105,000 ambao watakaa vizuri wanapokuwa wanatazama mpira. 

Alisema jana wamewasili eneo la Nzuguni litakalojengwa uwanja huo na wataalamu kutoka Morocco ambao wamekubaliana na michoro ya ujenzi ikiwamo eneo pia. 

Alifafanua zaidi ya kuwa Rais John Magufuli anataka hata kesho uanze na kuongeza; Magufuli alisema yuko tayari kuchangia chochote ili mradi uwanja ukamilike. 

"Kwa kweli hautachelewa tukikamilisha baadhi ya taratibu tu, zoezi la ujenzi linaanza," alisema Mfugale. 

Hata hivyo hakutaka kusema gharana za ujenzi huo na kuongeza zitajulikana baada ya kufanya uhakiki wake. 

Akuzungumzia eneo linalotarajia kujengwa, alisema ni zuri na linafaa kwa ujenzi huo wa kwanza. 

Aidha, mwakilishi kutoka Morocco, Soussi Yassir, aliipongeza serikali kwa kuteua eneo zuri la ujenzi huo. 

Alisema ujenzi utaanza haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha jiji linakuwa na uwanja wa michezo wa kisasa 
Alisema hawataiangusha serikali kwa kuwa wamejipanga vizuri kuitekeleza kazi yetu.

Habari Kubwa