Vita ya Waingereza Ligi ya Mabingwa Ulaya

16Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Nyon
Nipashe
Vita ya Waingereza Ligi ya Mabingwa Ulaya

TIMU za England, Tottenhan na Manchester City zimepangwa kuumana zenyewe kwa zenyewe kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika ratiba iliyopangwa jana mjini Nyon, Uswisi Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Ulaya, klabu zingine za England, Liverpool imepangwa kuumana na Porto, huku Manchester United ikipelekewa kwa Barcelona wakati mabingwa wa Italia, Juventus wenyewe wataumana na Ajax.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Spurs itakuwa nyumbani kuwaalika City Aprili 9, huku Liverpool ikiwa mwenyeji wa Porto, siku inayofuata Manchester United itakuwa nyumbani Old Trafford kuwakaribisha Barcelona wakati Juventus itaanzia nyumbani usiku huo kucheza na Ajax.

Awali timu za jiji la Manchester zote zilikuwa zicheze siku moja, lakini Uefa imefanya mabadiliko kwa mchezo wa Manchester United kuupeleka mbele siku moja ili kukwepa timu kutoka jiji moja kucheza siku moja.

Kwa namna ya ratiba hiyo ilivyo, mshindi wa mchezo kati ya Spurs dhidi ya Man City atakutana na mshindi kati ya Ajax na Juventus kwenye hatua ya nusu fainali wakati mshindi wa mchezo kati ya United na Barcelona atacheza na mshindi wa mchezo kati ya Liverpool na Porto.
Michezo ya marudio hatua hiyo ya robo fainali itafanyika Aprili 16 na 17.

Habari Kubwa