Viwanja tenisi kuboreshwa nchini

14Jan 2019
Renatha Msungu
Dar es Salaam
Nipashe
Viwanja tenisi kuboreshwa nchini

SHIRIKISHO la Tenisi la Kimataifa (ITF) limeipa Tanzania kiasi cha Dola za Marekani 20,000 (zaidi ya Sh. milioni 44) kwa ajili ya ukarabati wa viwanja vinne vya mchezo huo vilivyoko katika eneo la Gymkhana jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Tayari ukarabati wa viwanja hivyo ambavyo vitatumiwa katika kufundishia wachezaji chipukizi wa mchezo huo hapa nchini umeshaanza.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Chama cha Tenisi Tanzania (TTA), Denis Makoye, alisema mafunzo ya kuinua vipaji vya chipukizi yanatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu na kuongeza kuwa ukarabati unafanyika chini ya Kampuni ya BQ Contractor.

"Tumefurahi sana kuona tumepata fedha hizo na hii inatokana na baada yao TTA, Klabu ya Gymkhana kupanga kuanzisha kituo hicho cha mafunzo ya mchezo huo katika viwanja hivyo," alisema Makoye.

Kiongozi huyo alisema kuwa lengo la kukarabati viwanja ni kutaka kuona mchezo wa tenisi unakuwa hapa nchini kama ilivyo michezo mingine.

Aliongeza wazazi wanapaswa kuwapeleka vijana kupata mafunzo watakayoyatoa ili kusaidia kuvumbua vipaji vya wachezaji chipukizi ambao wamejificha kutokana na kutokujua nini wafanye ili wajiendeleze.

Naye Katibu wa TTA, Inger Njau, aliishukuru ITF na BQ kwa mchango wao waliutoa kwa ajili ya kuendeleza tenisi hapa nchini.

Meneja Maendeleo na Biashara wa BQ, Hili Bura, alisema huu ni mwanzo, wamejipanga kuendelea kushirikiana na TTA kuhakikisha mchezo wa tenisi unafanya vizuri ndani na nje ya Tanzania.

Habari Kubwa