Vodacom kurusha mashabiki Afcon Misri

11Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Vodacom kurusha mashabiki Afcon Misri

KUELEKEA msimu wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania (PLC),-

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara wa Vodacom, Linda Riwa.

Imezindua Kampeni ya Data na Afcon kupitia huduma ya "Soka Letu" na itawazawadia wateja wake 10 tiketi za kwenda kushuhudia timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ikicheza huko Misri.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika ofisi za makao makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara wa Vodacom, Linda Riwa, alisema huu ni wakati wa kusapoti vya nyumbani na kwamba kampeni hiyo itaendeshwa nchi nzima ili kutoa fursa kwa kila Mtanzania na shabiki wa Taifa Stars kushinda tiketi ya kwenda kuishangilia.

“Tunafuraha kubwa kuona timu yetu ya taifa imefuzu kuwania Kombe hili la Afcon, na tunasambaza furaha yetu kwa wateja wetu. Kama mnavyojua kwa takriban miaka 39 haikupata fursa ya kuwania mashindano haya, hivyo inabidi tuipe nguvu na kuishabikia.

"Kupitia huduma ya 'Soka Letu' kutoka Vodacom Tanzania, tutawazawadia wateja wetu 10 ambao ni mashabiki wa Taifa Stars tiketi za ndege pamoja na malazi huko Misri, ili wakaishangilie timu yetu ya taifa,” Riwa alisema.

Alisema kampeni hiyo ilianza rasmi siku hiyo (Juni 7) na itafungwa Juni 21, mwaka huu, ambapo washindi watatangazwa.

“Kuna zawadi kemkem katika msimu huu wa Kombe la Mataifa ya Africa kupitia Data na Afcon, hivyo ili ushinde inabidi ujiunge na huduma ya 'Soka Letu' kwa kubonyeza *149*84# na utapokea jumbe mbalimbali kuhusiana na mechi zinazoendelea.

"Na si hayo tu, kutazama mechi mubashara unahitaji kuwa na intaneti ya uhakika, hivyo endelea kujiunga na vifurushi vya intaneti upate hadi mara mbili ya kifurushi unachonunua 'Data Datani'," aliongeza Riwa.

Alifafanua kuwa kwa wateja wapya, watapata dakika tano bure za kupiga papo hapo, lakini pia wateja wote wanaweza kujishindia dakika 10,000 za kupiga kutoka Vodacom Tanzania PLC, na pia watapata nafasi ya kujibu maswali na kujishindia pointi nyingi zaidi, ambazo zitawawezesha kuingia katika droo ambayo washindi watapata tiketi za kwenda Misri, huku gharama zote zikiwa zimelipiwa na kampuni hiyo.

Kwa upande wa baadhi ya mashabiki wa Taifa Stars, Juma Hamisi wa Mbagala na Christian John wa Mwenge, waliipongeza Vodacom Tanzania kwa kuwa wadau wakubwa wa soka nchini. “Tunafurahi sana kuona Vodacom wakitusapoti kwa hili, nina imani washindi watakaopatikana wataongeza ushabiki kule Misri na kututia nguvu ya kufanya vizuri katika msimu huu,” alisema Hamisi.

Habari Kubwa