Vunjabei aimwagia Simba bilioni mbili

21Apr 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Vunjabei aimwagia Simba bilioni mbili

UONGOZI wa Klabu ya Simba umeonyesha thamani ya ukubwa wake baada ya jana kuingia mkataba wa mabilioni ya shilingi na Mfanyabiashara wa Kitanzania, Fred Ngajiro maarufu kama Fred Vunjabei, kupitia Kampuni yake ya Vunjabei Group kwa ajili ya kutengeneza na kusambaza jezi na vifaa vingine vya michezo.

Mkataba huo ambao ni wa miaka miwili, unathamani ya Sh. bilioni mbili, hivyo kuifanya Simba kuwa klabu ya kwanza Afrika Mashariki na Kati kuingia mkataba mnono kama huo kwa upande wa jezi na vifaa vingine vya michezo.

 

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez, alisema Desemba mwaka jana walitangaza tenda hiyo na kujitokeza kampuni 11 binafsi, lakini Fred Vunjabei ndiye aliyeshinda.

Alisema uamuzi wa kumtangaza Vunjabei ni kuwapa fursa wafanyabiashara Watanzania ambao watatoa ajira kwa vijana waliopo mitaani kutangaza bidhaa za Simba kupitia tenda hiyo.

"Tumeingia makubaliano na Vunjabei kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh.bilioni mbili ni tofauti na msimu uliopita ambao awali aliyeshinda tenda hiyo alitoa kiasi cha Sh. Milioni 100," alisema Barbara.

Kwa upande wa Fred Vunjabei, alisema kupitia mkataba huo ana uhakikisha wa kufanya biashara na Simba kwa kuzingatia malengo ikiwamo kusambaza bidhaa bora na uhalisia wa hali ya juu yenye nembo ya klabu hiyo.

Alisema mkataba huo umelenga timu zao zote ikiwamo vijana, wanawake na timu kubwa ambayo inawakilisha vema Tanzania kwenye michuano ya kimataifa wakati huu ikiwa imetinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Kupitia mkataba huo tutaenda kila mkoa kufungua duka la vifaa vya nembo ya Simba kwa kulipa kodi ya serikali, hivyo tutakuwa makini na kuwachukulia hatua wale wanauza jezi feki," alisema Fred Vunjabei.

Habari Kubwa