Waamuzi waahidi haki Ligi Kuu

06Sep 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Waamuzi waahidi haki Ligi Kuu

KAMATI ya Waamuzi nchini, imesema kuwa waamuzi wote wako tayari kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21, na kuahidi watachezesha kwa kufuata sheria zote na kanuni zake, huku wakiwa fiti kimwili na kiakili.

Mwenyekiti wa Waamuzi, Sudi Abdi amesema kuwa wameshajipanga kuhakikisha wanapunguza matatizo yale yaliyokuwa wanajitokeza siku za nyuma na kuwatoa shaka mashabiki wa soka nchini kutarajia uchezeshaji wa hali ya juu.

"Tumewapa semina waamuzi wetu, tumewapima utimamu wa mwili, tumewafanyisha mazoezi uwanjani na darasani pia, tumewapima uelewa na pia tumewaangalia nyuma walifanya nini." alisema Sudi, mwamuzi wa Kimataifa nchini Tanzania.

Alisema kuwa mwanzo mwa Ligi Kuu wanatarajia kuanza na waamuzi ambao walifanya vema msimu uliopita.

Aliwahakikishia Watanzania kuwa makosa yatapungua kwa sababu na hata pale yatakapokuwa yanajitokeza, basi hawatosita kuyafanyia kazi.

"Waamuzi wako vema na watachezesha vizuri kuendana na wakati kwa sababu mabadiliko ya kanuni yao yanatokea mara kwa mara, lakini naamini kila timu kitakwenda vizuri," alisema mwenyekiti huyo.

Kuhusu kupata haki yao, Sudi alisema suala hilo haliko mikononi mwake, lakini akasema kuwa anaamini waamuzi watakuwa wanapata haki yao kama kawaida.

Ligi Kuu Tanzania Bara inaanza leo kwa mechi sita kupigwa, huku mechi tatu zikichezwa kesho Jumatatu.

Habari Kubwa