Wabunge wapinga serikali kuingilia uchaguzi wa TFF

11Jun 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Wabunge wapinga serikali kuingilia uchaguzi wa TFF
  • ***Tarimba, Ally Mayay nao wachukua fomu kumvaa Karia urais, huku sasa...

WAKATI wagombea wa nafasi ya kiti cha urais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), wakiongezeka kutoka watano wa juzi na hadi saba baada ya nguli na mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay Tembele na aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Tarimba Abbas kuchukua fomu jana, baadhi ya wabunge ....

wameibuka kupinga maoni ya wenzao kuhusiana na kuitaka serikali kuingilia mchakato wa uchaguzi huo.

TFF inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu Agosti 7, mwaka huu huko jijini Tanga kwa kutumia katiba mpya iliyopitishwa mwaka juzi ambapo nafasi zinazowaniwa ni kiti cha urais na Wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji.

Vuguvugu la kutaka serikali kuingilia mchakato wa uchaguzi huo, lilianzishwa na Mbunge wa Kinondoni (CCM), Tarimba pamoja na Mbunge wa Jimbo la Mwera mjini Zanzibar, Zahor Mohammed Haji, ambaye alichukua fomu siku ya kwanza ya dirisha hilo, Jumanne wiki hii.

Wabunge hao kwa pamoja walitoa kilio chao wakiitaka serikali kuingilia kati mchakato huo kwa kile walichodai kuwa kuna rafu mbaya imechezwa na mgombea mmoja kwa kuziba nafasi za kupata wadhamini ili kuwa mgombea pekee.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula, alisema TFF inapaswa kuachwa iendelee na mchakato wake wa uchaguzi kwa kutumia chombo chake huru na serikali isiingilie kama ambavyo wadau wengine wa michezo walivyoshauri.

Mabula alisema anaamini TFF ina chombo chake huru kitakachosimamia uchaguzi huo kwa haki na kwa kufuata kanuni na sheria zilizowekwa na zinazotambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na duniani (FIFA).

Alisema bado wadau wa michezo wanatamani kuona kiwango cha mchezo huo unaopendwa na mashabiki wengi duniani unazidi kupata maendeleo hapa nchini na kwa kuzingatia hilo anashauri mchakato huo usiingiliwe na serikali.

"Hatutamani kuona serikali inaingia katika mchakato huu, inaingia katika jambo hili, TFF inachombo chake ambacho kinaongozwa na taratibu zilizonyooka na ziko vizuri, kuitaka serikali isiingilie ni kuitaka TFF isifike kule kunakokusudiwa, tuache mchakato huu kama ambavyo hatutaki serikali isiingilie vyama vingine," alisema Mabula.

Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Timotheo Mzava, alisema kwa sasa wadau wanataka kuona mpira wa Tanzania ukiendelea kusonga mbele na miaka ya nyuma kulikuwa na migogoro kwa sababu ya mivutano isiyokuwa na tija, hivyo huu si wakati sahihi wa kuitaka serikali kuingilia uchaguzi na badala yake tutaipeleka nchi mahali ambako tutapajutia.

"Hoja ya 'Endorsement' (kuidhinishwa/kudhaminiwa), isichukulie kama sababu na ikaleta mambo ya kutuvuruga, hii ipo kuanzia katika chaguzi za CAF na FIFA, hata katika vyama vya siasa pia, uhuru wa kudhaminiwa na kupata dhamana ni hiari," alisema Mzava.

Mbunge huyo aliongeza kwa kuwataka wagombea na wadau wa soka kusubiri hadi siku ya mwisho ya kurejesha fomu ambapo watafahamu wagombea waliokidhi vigezo maana wapo wengine waliochukua fomu kupitia mtandaoni na hivyo hawajulikani.

"Mwaka 2019 kulikuwa na uchaguzi wa Fifa na Infantino (Gianni), alipita bila kupingwa kwa sababu alipata 'Endorsement' kutoka katika nchi zote, tuache mchakato wa uchaguzi wa TFF uendelee kwa mujibu wa kanuni na sheria zake, niwaombe wanasiasa wauache, juzi serikali iliahirisha mechi wakapiga kelele, leo watu hao hao wanaitaka serikali iingilie kati, wanashangaza," alisema Mzava.

Naye Mbunge wa Handeni (CCM), Hamisi Mwinjuma maarufu "Mwana FA" alisema ni vyema sheria zinazosimamia mpira zikafuatwa na si kwenda kinyume.

"Kama mtu amedhaminiwa na watu wote aachwe, serikali hii hii iliyokataliwa wiki mbili zilizopita leo wanaita ikaingilie uchaguzi? Endorsement sio kitu kipya? Ilitokea kwa Infantino na ni hiari," Mwana FA alisema.

Vuma Augustine, Mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), alisisitiza kanuni na taratibu zifuatwe katika kuendesha mchakato huo kwa sababu mpira wa miguu unabeba hisia kali za mamilioni ya mashabiki.

"Serikali kuingilia uchaguzi, tutapotea njia, tusiende kuharibu hisia za watu wengi, tutakuwa vituko, kama kuna 'rafu' basi zishughulikiwe huko huko kwa kufuata taratibu za mpira," alisema mbunge huyo.

Mbali na Tarimba na Mayay waliochukua fomu jana, wengine ambao tayari walishachukua katika nafasi hiyo ya urais ni Deogratius Mutungi, Evans G. Mgeusa, Oscar Oscar, Zahor Mohammed Haji na Karia anayetetea kiti hicho.

Kwa upande wa nafasi ya Kamati ya Utendaji ni Lameck, Nyambaya, Liston Katabazi na Michael Petro, Sandy Mohamed Kimji na Athuman Kingome Kambi (Kanda namba 1- Dar es Salaam, Lindi, Morogoro, Mtwara na Pwani), mwingine ni Khalid Abdallah (Kanda namba 2- Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga) huku Mohamed Aden na Osuri Kosuri wakichukua fomu kwa (Kanda namba 4 - Dodoma, Shinyanga, Simiyu na Singida) na Salum Umande Chama akiwa ni kwa (Kanda namba 5 - Geita, Kagera, Mara na Mwanza).

Habari Kubwa