Wagombea TFF wapigana vikumbo jijini Mwanza

16Jul 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Wagombea TFF wapigana vikumbo jijini Mwanza

WAGOMBEA wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), utakaofanyika Agosti 12, mwaka huu, wanapishana huku na kule kusaka kura kwa wajumbe walioko jijini hapa, gazeti hili limebaini.

Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida wagombea hao wanadai kuwa wamekuja kuangalia mechi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), ambayo mwenyeji Taifa Stars aliikaribisha Rwanda hapo jana, lakini ukweli ni kufanya kampeni za chini kwa chini.

Mmoja wa wagombea hao ambao wako jijini hapa na si kiongozi aliyeko madarakani ni mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Imani Madega, ambaye anawania Urais wa TFF na Benista Lugola anayewania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda ya Shinyanga/ Geita.

Viongozi ambao wako madarakani na ni wagombea ni pamoja na Kaimu Makamu Rais, Wallace Karia, anayegombea nafasi ya Urais, James Mhagama na Elias Mwanjala wanaowania ujumbe.

Pia "wapambe" wa baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo nao wako jijini hapa kwa ajili ya kuwaombea kura wagombea wao kwa kufanya vikao mbalimbali.

"Kazi ipo hapa, naona Stars imesaidia kuwakutanisha wagombea na wapiga kura," alisema mwenyeviti wa Chama cha Soka cha mkoa mmoja ( jina tunalihifadhi).

TFF inatarajia kufanya uchaguzi baada ya viongozi wake waliochaguliwa Oktoba 2013 kumaliza muda wao kwa mujibu wa katiba ya shirikisho hilo ambapo muda wa kukaa madarakani ni miaka minne.

Habari Kubwa