Wagombea ZFF wazidi kujinadi

01Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Wagombea ZFF wazidi kujinadi

IKIWA leo ndio mwisho wa kufanya kampeni kwa wagombea wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), mgombea Urais, Seif Kombo Pandu, amesema endapo atachaguliwa kuliongoza shirikisho atahakikisha anadhibiti vitendo vya rushwa michezoni.

Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), mgombea Urais, Seif Kombo Pandu.

Pandu alisema kuwa anataka kumaliza vitendo vya rushwa katika mchezo wa soka kwa sababu vinachangia kudidimiza vipaji kwa wachezaji wao na timu iliyo na kiwango kizuri kukosa nafasi ya kutwaa mataji mbalimbali.

Hata hivyo Pandu alisema kuwa waamuzi wanaochezesha ligi mbalimbali visiwani hapa wamekuwa wakilalamikiwa kwa sababu ya tatizo la kutolipwa madeni yao kwa wakati.

"Tatizo la ukata kwa waamuzi au vilabu vinavyopokea au kujihusisha na rushwa, waamuzi wanacheleweshewa malipo yao, lakini vilabu pia vingi vinakumbwa na umasikini, kwa hiyo tatizo hilo mimi nitalishughulikia hadi litamakizika, " alisema Pandu.

Aliongeza kuwa katika kumaliza tatizo hilo, atahakikisha anashirikiana vema na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Zanzibar, Jeshi la Polisi huku wakijipanga kuwalipa posho zao kwa wakati waamuzi wote wanaocheza mechi zinazosimamiwa na shirikisho hilo.

Alisema pia atahakikisha vilabu vyote vinavyoshiriki Ligi Kuu Zanzibar vinakuwa na leseni kama kanuni na sheria za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na FIFA inavyoelekeza.

Naye Mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais, Salim Ubwa kutoka Pemba amesema endapo atachuguliwa katika nafasi hiyo atahakikisha anashirikiana rais katika kuboresha soka la Zanzibar ili liwe lenye hadhi na hamasa.

Ubwa alisema soka la Zanzibar hivi sasa limepoteza hamasa kwa mashabiki hali inayopelekea idadi ya mashabiki wabaojitokeza uwanjani kushuhudia mechi mbalimbali hususani zile za Ligi Kuu kupungua.

Aliongeza kuwa ili kupata mafanikio, akiingia madarakani atadumisha ushirikiano kati ya ZFF na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara ya michezo.

ZFF inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu kesho kwa kutumia katiba mpya iliyosajiliwa mapema mwaka huu.

Habari Kubwa