Wakenya wang'ara Rock City Marathon, serikali yafunguka

22Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
Wakenya wang'ara Rock City Marathon, serikali yafunguka

WAKATI msimu wa kumi wa mbio za Rock City Marathon ukihitimishwa kwa kushirikisha mamia ya wanariadha kutoka ndani na nje ya nchi, serikali imesema ipo haja ya kufanya tathmini ili kupima mchango wa mbio za aina hiyo katika kuinua sekta ya utalii hapa nchini ili iweze kuwekeza nguvu zaidi katika....

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla (katikati) akitoa zawadi ya fedha taslimu kiasi cha Sh. milioni nne kwa mshindi wa mbio za Rock City Marathon Km. 42, kwa upande wa wanawake, Elilither Tamui kutoka Kenya aliyeibuka mshindi baada ya kutumia muda wa saa 2:42:50. Wengine ni pamoja na Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta ya TIPER, Emmanuel Kondi (kulia), ambao ni miongoni mwa wadhamini wakubwa wa mbio hizo zilizofanyika mwishoni mwa wiki kwenye viunga vya jengo la biashara la Rock City Mall jijini Mwanza. MPIGAPICHA WETU

kuziboresha.

Akizungumza wakati wa kilele cha mbio hizo zilizofanyika kwenye viunga vya jengo la biashara la Rock City Mall, jijini Mwanza mwishoni mwa wiki, ambapo ilishuhudiwa wanariadha kutoka nchini Kenya wakiendelea kutamba, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alisema wingi wa wawashiriki kutoka ndani na nje ya nchini ni kiashirio tosha kuwa mbio hizo zikitumika vizuri kutangaza utalii zitachochea ukuaji wa sekta hiyo muhimu kiuchumi.

“Nimeshuhudia mamia ya washiriki kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini wamekuja kushiriki mbio hizi, tayari hiyo ni sehemu ya utalii wa ndani. Zaidi imeshuhudiwa ushiriki wa wenzetu kutoka nje ya nchini ikiwamo Kenya, Rwanda na wengine nje ya Bara la Afrika nao wamekuja.”

“Ili kupata mchango hasa wa mbio kama hizi kwenye Sekta ya Utalii na ukuaji wa uchumi naagiza ufanyike utafiti wa kisayansi ili serikali tujue namna ya kuziunga mkono ziendelee kufanya vizuri zaidi,’’ aliagiza Dk. Kigwangalla ambaye alishiriki kukimbia mbio za Km. 21.

Tangu kuanzishwa kwa mbio miaka 10 iliyopita zimekuwa zikivutia zaidi washiriki kutoka mataifa ya Kenya na Rwanda ambapo ilishuhudiwa mwanariadha kutoka Kenya, Ibrahimu Too akiibuka mshindi wa mbio za Km. 42 upande wa wanaume baada ya kutumia muda wa saa 2:18:34 akifuatiwa na Wakenya wenzake Willium Koskei na John Muthui waliotumia muda wa saa 2:19:06 na 2:21:30 kila mmoja.

Mtanzania pekee kwenye 10 bora wanaume alikuwa Hamis Athumani aliyefanikiwa kushika nafasi ya nne huku akitumia muda wa saa 2:21:36.

Kwa upande wa wanawake katika mbio hizo za Km. 42 ilishuhudiwa mwanariadha Elilither Tamui kutoka Kenya akiibuka mshindi baada ya kutumia muda wa saa 2:42:50 akifutiwa na Wakenya wenzake Joan Rotich (2:46:07) na Lydia Wafula (2:48:57) ambapo Watanzania Fabiola John na Zainabu Hamis walifanikiwa kushika nafasi ya sita na ya 10.

Katika mbio za Km. 21, mshindi wa kwanza upande wa wanaume ni Bernard Musau kutoka Kenya aliyetumia muda wa saa 01:11:26 akifuatiwa na Ochieng Julius kutoka Uganda aliyetumia muda wa saa 01:11:36 huku mshindi wa tatu akiwa ni Alex Nizemana kutoka Rwanda akitumia muda wa saa 01:12: 21.

Kwa upande wa wanawake katika mbio hizo za Km. 21 mshindi wa kwanza hadi wa nne wote ni kutoka Kenya ambao ni Ester Kakuri aliyetumia muda wa saa 1:21:44 , Vane Nyaboke (1:22:13), Ronah Nyabochoa (1:23:10) na Martha Njoroge (1:23:17), huku mshindi wa tano ni Grace Jackson kutoka Tanzania aliyetumia muda wa saa 1:24:23.

Akizungumzia matokeo hayo Mshauri wa Masuala ya Ufundi wa mbio hizo, John Bayo pamoja na kuwapongeza wanariadha kutoka Kenya kwa kufanya vizuri alisema Tanzania haikupata ushiriki wa wanariadha wakubwa kutokana na wengi wao kushiriki kwenye mbio za kimataifa na hivyo kutoa mwanya kwa wanariadha hususan wa Kenya kuweza kutamba kwenye mbio hizo.

Mbio hizo zilipambwa na burudani mbalimbali zikiwamo ngoma za asili na maonyesho ya wadau mbalimbali wa utalii pamoja na wadhamini wa mbio hizo ikiwamo Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) sambamba na Kampuni za TIPER na Pepsi.

Wadhamini wengine ni pamoja na, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), CF Hospital, Metro FM, Mwanza Water, Pigeon Hotel, The Cask and Grill, SDN na Kampuni ya Ulinzi ya Garda World.

Habari Kubwa