Wakongo wamtaja Samatta, Msuva

27Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wakongo wamtaja Samatta, Msuva

WAKATI timu ya soka ya Taifa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ikiwahofia washambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samatta na Simon Msuva wanaocheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji na Morocco, kwenye mechi ya kimataifa ya kirafiki leo, Stars itamkosa kipa wake chaguo la kwanza, Aishi Manula.

Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Suleiman Morocco

Kipa huyo pia aliukosa mchezo uliopita wa kirafiki dhidi ya Algeria kutokana na matatizo ya enka yanayomkabili, hivyo hatacheza katika mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Taifa leo.

Akizungumza jana jijini, Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Suleiman Morocco, alisema kuwa Manula bado ni mgonjwa, lakini akiahidi watashuka uwanjani kusaka ushindi katika mchezo huo utakaofanyika kuanzia saa 10 jioni.

Morocco alisema wamejiandaa kukabiliana na ushindani kutoka kwa wageni wao na wametumia mchezo dhidi ya Algeria kama sehemu ya maandalizi ya kusaka ushindi watakapocheza na DRC.

"Hatuhitaji kupoteza tena mechi hii hapa nyumbani, tunajua itakuwa ngumu, lakini tuko tayari kupambana na kushinda," alisema kocha huyo mwenyeji wa Zanzibar.

Naye Kocha Ibenge Ikwange wa DRC, alisema kuwa anaamini kikosi chake kitakutana na upinzani kutoka kwa Taifa Stars ambao ina mchanganyiko wa wachezaji wanaocheza ndani na nje ya nchi.

"Natarajia mechi itakuwa nzuri, yenye burudani kutoka kila upande, siifahamu vizuri Tanzania, lakini najua kuna Samatta, Msuva, " alisema kwa kifupi Ikwange katika mkutano na waandishi wa habari jana.

Nahodha wa timu hiyo, Berik Afobe, alisema haifahamu Taifa Stars, lakini yeye na wachezaji wenzake wamejiandaa kucheza vizuri ili wapate ushindi na wanafurahia kupata nafasi ya kujipima na wenzao wa Tanzania.

Katika mechi iliyopita ya kirafiki, Taifa Stars iliyoko chini ya Kocha Mkuu, Salum Mayanga, ilifungwa mabao 4-1 wakati wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa 7-0 dhidi ya Waarabu hao kwenye mechi iliyopita kabla ya mchezo huo.

 

Habari Kubwa