Wakuogelea Madola watangazwa

14Nov 2017
Renatha Msungu
Nipashe
Wakuogelea Madola watangazwa

Chama cha Mchezo wa Kuogelea nchini (TSA), kimeteuwa wachezaji wanne watakaounda timu ya Taifa ambayo itaiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika Gold Coast, Australia Aprili mwakani.

Katibu Mkuu wa TSA, Ramadhani Namkoveka.

Wachezaji waliochaguliwa na TSA ikishirikisha kamati yake ya ufundi ni Celina Itatiro na Sonia Tumiotto kwa upande wa wasichana, upande wa wavulana ni Hilal Hilal na Collins Saliboko.

Katibu Mkuu wa TSA, Ramadhani Namkoveka, aliliambia gazeti hili jana kuwa wachezaji hao wamechaguliwa kutokana na viwango vyao walivyonyesha mwaka huu katika Mashindano ya CANA Kanda ya Tatu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi uliopita.

Alisema wachezaji hao ni sehemu ya timu ya kuogelea ambao wanaandaliwa na TSA kwa lengo la kuweza kufuzu mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika Japan mwaka 2020.

Namkoveka, alitoa wito kwa makocha wanaowaandaa wachezaji hao kuzidi kuwapa mazoezi ya kutosha ili kuweza kufikia kiwango kilichowekwa na Shirikisho la Kuogelea la Dunia (FINA).

"Wachezaji wote wapo katika mazoezi chini ya makocha wao. Hilal yupo Dubai, Collins Saliboko na Sonia wako Uingereza wakifanya mazoezi na kuendelea na masoma," alisema katibu huyo huku akieleza kuwa kwa upande wa Celina yupo hapa nchini akiendelea na mazoezi chini ya makocha Kanisi Mabena na Michael Livingstone.

Habari Kubwa