Wanariadha 28 kuchuana Nyika

15Jan 2019
Renatha Msungu
Dar es Salaam
Nipashe
Wanariadha 28 kuchuana Nyika

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limesema kuwa litapeleka wanariadha 28 kushiriki mashindano ya kimataifa ya mbio za Nyika yanayotarajiwa kufanyika Machi 31 mwaka huu nchini Denmark, imeelezwa.

Katibu wa RT, Wilhelm Gidabuday, alisema wanariadha watakaoenda katika mashindano hayo ni wale watakaofanya vizuri kwenye mbio za Kilimanjaro Marathoni zitakazofanyika mapema Machi mwaka huu.

Gidabuday alisema katika mashindano hayo wanariadha wanawake na wanaume watakimbia umbali wa kilomita 10, ambapo watachujwa na kubaki wanariadha 12 ambao watakwenda Dermark.

Aliongeza kuwa wanariadha wengine vijana 12 watakimbia mbio za vijiti na kuongeza kwamba wanariadha wote watakaofanya vizuri watapata nafasi katika timu itakayokwenda Dermark.

Alisema pia baadhi ya wanariadha watakaopata nafasi ya kupeperusha bendera ya nchi watagharamiwa na RT na wengine watalipiwa mahitaji yao na Shirikisho la Riadha la Kimataifa.