Wanariadha Dar kuchuana Uhuru

04Jul 2020
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Wanariadha Dar kuchuana Uhuru

WANARIADHA kutoka klabu mbalimbali wanatarajia kuchuana katika mashindano ya wazi yatakayofanyika leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini, Dar es Salaam imefahamika.

Wanariadha wa klabu mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam, wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa jijini ili kujiandaa na mashindano ya taifa yanayotarajiwa kufanyika Septemba, mwaka huu. PICHA : JUMANNE JUMA

Akizungumza na gazeti hili jana ,Kocha Mkuu wa timu ya riadha mkoa wa Dar es Salaam, Idd Muhunzi, alisema lengo la mashindano hayo ni kuangalia uwezo wa kila mchezaji baada ya kukaa muda mrefu kutokana na kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona.

"Mashindano hayo yatashirikisha klabu mbalimbali zikiwamo zile timu za Umiseta ambazo zilishiriki mashindano ya Taifa mwaka jana," alisema Muhunzi.

Kocha huyo alisema wachezaji watakaokuwa na uwezo mzuri watapata nafasi ya kushiriki katika mashindano ya Taifa yatakayofanyika kuanzia September 5 na 6, mwaka huu.

" Ugonjwa wa corona ulituvurugia mipango mingi, isipokuwa bado naamini wachezaji wangu watakuwa katika kiwango bora kama awali, licha ya kukaa muda mrefu bila kushiriki mashindano yoyote," Muhunzi alisema.

Aliwataka wadau wa mchezo huo kujitokeza kushuhudia wachezaji watakaokuwa wanashiriki mashindano hayo ili kuongeza hamasa katika mchezo huo.

Habari Kubwa