Wanariadha mashuhuri kuchuana Tulia Marathon

07Mar 2017
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Wanariadha mashuhuri kuchuana Tulia Marathon

WANARIADHA kutoka kila kona nchini wanatarajia kuonyeshana kazi kwenye nusu marathoni [kilomita 21] yaliyoandaliwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Akson, kupita Shirika la Tulia Trust.

Akizungumza na wandishi wa Habari jana kuhusu maandalizi ya mbio hizo, Katibu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Mbeya, Lwiza John, alisema mashindano hayo yatafanyika Machi 11 mwaka huu jijini Mbeya.

Lwiza alisema mbio hizo zitaanzia katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya mpaka Stendi ya Mabasi ya Nane nane na kurudi tena Sokoine.

Aliwataja baadhi ya wanariadha watakaoshiriki kuwa ni pamoja Dickson Marwa, Reginald Lucas, kutoka Arusha na wengine Banuelia Brighton, Osward Revelian, Jacob Raimond.

Lwiza alisema lengo la mashindano hayo ni kupata fedha kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya na elimu hususan uboreshaji majengo na vyoo katika sekta hizo.

“Tulia Marathon lengo lake ni kukusanya fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya na elimu, maeneo yanayolengwa kwenye afya ni Kituo cha Afya cha Ruanda kilichopo Mwanjelwa na Hospitali ya Wilaya ya Rungwe Makandana ambako utafanyika uboreshaji wa wodi ya wazazi,”

“Katika Elimu maeneo yanayokusudiwa kuboreshwa ni pamoja na Shule ya Wasichana ya Loleza ambayo itafanyiwa maboresho kwenye mabweni mawili na vyoo pamoja na shule tatu za msingi,” alisema Lwiza.

Alitaja zawadi kwa washindi wa mbio hizo kuwa mshindi wa kwanza atapata kitita cha Sh. milioni moja wa pili Sh. 700,000 na wa tatu atapata Sh. 500,000.

Aidha, alisema kutakuwa na shindano la mbio fupi za kilomita mbili ambazo zitawahusisha wabunge mbalimbali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwamo Naibu Spika mwenyewe na kwamba katika kipengele hicho hakutakuwa na zawadi kwa mshindi.

Kadhalika, alisema kutakuwa na mashindano mengine ya kilomita tano ambayo yatahusisha makundi mbalimbali wakiwamo walemavu, wazee na watoto ambayo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya Sh. 100,000, wa pili Sh. 70,000 na wa tatu atajinyakulia Sh. 50,000.

Lwiza aliwataka wananchi mbalimbali kuhudhuria kwenye mashindano hayo kwa wingi ili kushuhudia wanariadha hao wakionyeshana uwezo.

Habari Kubwa