Waogeleaji wapata udhamini kusaka tiketi ya Olimpiki

04May 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Waogeleaji wapata udhamini kusaka tiketi ya Olimpiki

​​​​​​​KAMPUNI ya Greatlakes Freight & Transport, imepiga tafu waogeleaji wa Tanzania wanaowania nafasi ya kufuzu mashindano ya Olimpiki yaliyopangwa kufanyika mjini Tokyo, Japan kuanzia Julai 23 hadi Agosti 8, mwaka huu.

Waogeleaji wa Tanzania kutoka kushoto, Hilal Hilal, Austin Okore na Collins Saliboko wakiwa nchini Afrika Kusini tayari kwa mafunzo ya kuogelea ya Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea la Afrika (Cana) na baadaye Mei 7 na 8, mwaka huu kushindana kuwania nafasi ya kufuzu mashindano ya Olimpiki. MPIGAPICHA WETU

Waogeleaji hao wawili, Collins Saliboko na Hilal Hilal, wamechagulia na Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), kusaka tiketi ya kuwania kufuzu mashindano ya Olimpiki yaliyopangwa kufanyika Mei 7 na 8 mjini Stellenbosch, Afrika Kusini.

Wakati Collins amedhaminiwa kuanzia mazoezi ya gym na kwenye maji, Hilal ambaye alikuwa mazoezini Dubai, amedhaminiwa tiketi ya kwenda Afrika Kusini kushiriki katika mashindano hayo na iwapo watafuzu, waogeleaji hao watashiriki katika mashindano hayo ya Tokyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Greatlakes Freight & Transport, Fahmy Ahmed, alisema jana kuwa wameamua kusaidia mchezo wa kuogelea ili kuleta hamasa katika mchezo huo na maendeleo kwa vijana.

Fahmy alisema wamedhamini waogeleaji hao kama sehemu ya kampuni kujihusisha na shughuli za kijamii, kuendeleza vipaji vya vijana wa leo na kuhamasisha mchezo huo.

Pia wanahamasisha kampuni nyingine kuwaunga mkono vijana wetu, ili waweze kupeperusha bendera ya Tanzania bila vikwazo na mawazo yanayoweza sababishwa na upungufu wa mazoezi na vifaa stahiki.

Alisema mchezo wa kuogelea una vipaji vingi nchini na pia unatazamwa zaidi katika mashindano ya Olimpiki.

Alisema kwa hapa nchini, mchezo huo unashindwa kuendelea kutokana na kukosa sapoti kutoka kwa jamii na hasa udhamini.

“Kampuni nyingi zinapendelea zaidi kudhamini michezo maarufu, kama mpira wa miguu na ngumi na kuona mchezo wa kuogelea hauna tija na wala haufahamiki," alisema.

Aidha, amewashauri watu kuweka bidii kwenye mchezo huo kwa kuwa una waogeleaji wengi ambao wanaweza kuitangaza nchi nje ya mipaka yake.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa TSA, Asmah Hilal, aliipongeza kampuni hiyo kwa msaada mkubwa na kuwawezesha waogeleaji hao kujiandaa na kwenda kushindana kuwania nafasi ya kufuzu Olimpiki.

Asmah pia alitoa shukrani kwa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na duka la kuuza vifaa vya michezo la Just Fit kwa kusaidia waogeleaji hao.  

Habari Kubwa