Waomba muda kuongezwa kushiriki mashindano

01Dec 2021
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe
Waomba muda kuongezwa kushiriki mashindano

WARATIBU na washiriki wa michezo kutoka kanda mbali mbali nchini wanaoshiriki mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa vyuo vya Ualimu Tanzania, yanayofanyika kitaifa mkoani Mtwara, wameiomba serikali kupitia wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia, kuongeza muda wa siku za kushiriki pamoja ...

na idadi ya washiriki kwa kila kanda.

Wamesema idadi ya washiriki na siku za kushiriki zikiongezwa zitatoa fursa zaidi kwa washiriki kuonyesha vipaji vyao kwa kuwa watakuwa wanashiriki michezo michache tofauti na sasa ambapo mwanamichezo mmoja anaweza kushiriki michezo zaidi ya miwili kwa siku moja

Wakizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa baada ya kumalizika kwa mchezo wa volebali uliowakutanisha kanda ya kusini na Kaskazini, waratibu hao wakiongozwa na Mwalimu Amicha Igogo kutoka chuo cha Ualimu Monduli, walisema idadi ndogo ya washiriki imesababisha mchezaji mmoja kushiriki michezo mingi kwa wakati mmoja hali inayominya fursa ya kuonyesha vipaji halisi walivyo navyo .

“Hivi vipaji vinavyoonekana hapa nina hakika vingejidhihirisha zaidi kama kila mmoja angeshiriki michezo michache na kuwa na muda wa kutosha wa kupumzika kabla ya mchezo mwingine, tunashauri michezo ijayo waandaaji waliangalie jambo hili kwa ajili ya kuleta tija zaidi”amesema Amicho

Medard Kyobya mratibu wa Umisavuta na mratibu wa michezo kutoka kanda ya Ziwa alisema tokea michezo hiyo ianze Novemba 28 mwaka huu, ameridhishwa na namna waamuzi wanavyotekelezajibu wao naa kuwaomba wadau wa michezo hususan soka kuwatupia jicho kwa ajili ya manufaa ya Taifa kwa siku zijazo

Amesema katika michezo hiyo amebaini vipaji vingi ikiwemo umakini wa marefa na kuomba waendelezwe kwa ajili ya kukabilioana na changamoto ya kila siku ya kuwa na marefa wasiotokeleza wajibu wao ipasavyo.

“Mimi ni mwanamichezo na mwalimu wa michezo kwa kweli hapa nimebaini vipaji vingi wakiwemo marefa ninawashauri watu wanaotafuta vipaji vya michezo mbali mbali watumie nafasi hii kuwaendeleza hawa vijana,” alisema Kyobya.

Mratibu wa Umisavuta Kitaifa kutoka wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Mwalimu Laurance Mselenga,alisema wamepokea maoni ya washiriki wa kanda mbali mbali juu ya muda na idadi ya washiriki na kuahidi kuongeza idadi ya washiriki na uda wa mashindano

Alisema kwa sasa michezo inayoendelea mkoani Mtwara kuna jumla ya michezo 13 ambayo kila kanda inapaswa kushiriki hali inayofanya wachezaji waliopo katika kanda husika kushiriki ichezo mingi

“Tumeliangalia hili kwa umakini, kama mnavyojua michezo hii ilikuwa haijafanyika kwa muda mrefu mpaka mpaka mwaka juzi yaliporejeshwa rasmi hivyo hizi changamoto tunazifanyia kazi ninaamini wakati ujao tutakuwa tumepiga hatua kubwa zaidi na hata idadio ya washiriki inaweza kuongezeka kwa kila kanda kutoka idadi ya sasa ya wanamichezo 95”alisema Mselenga

Mashindano ya Umisavuta ilizinduliwa Novemba 29 Mwaka huu na Naibu waziri wa Utamaduni sanaa na michezo, Pauline Gekuli, aliyemuwakilisha waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, ikiwa na jumla ya wanamichezo 665 kutoka kanda saba za nchi na inatarajiwa kufikia tamati Disemba 5 mwaka huu.

Habari Kubwa