Wapinzani wa Yanga wamnasa kocha mpya

03Mar 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Wapinzani wa Yanga wamnasa kocha mpya

WAKATI Yanga ikijipanga kuongeza kasi katika safari yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wapinzani wao watakaokutana nao wiki ijayo, APR ya Rwanda wanatarajia kumtangaza kocha mpya wakati wowote kuanzia sasa.

Kikosi cha timu ya APR kutoka Rwanda.

Kocha huyo raia wa Tunisia, Nizar Khanfir mtihani wake wa kwanza utakuwa katika mechi dhidi ya Yanga mjini Kigali, Jumamosi wiki ijayo.

Taarifa ambazo gazeti hili imezipata jana kutoka Kigali, zinadai kuwa kocha huyo aliyewahi kuifundisha timu ya Taifa ya Tunisia, amekubali kujiunga na miamba hiyo ya soka Rwanda.

Inadaiwa kuwa tayari kocha huyo aliyewahi pia kufundisha timu ya Stade Gabesien ameaga nchini kwao na anajiandaa kujiunga na timu hiyo ya Rwanda mali ya jeshi.

Anatua APR kuchukua mikoba ya kocha aliyetangulia, Dusan 'Dule' Suljagic na anasaidiana kocha Mnyarwanda, Emmanuel Rubona.

Wakati huohuo, Msemaji wa Yanga, Jerry Muro alisema jana kuwa timu hiyo itaondoka nchini Alhamisi ijayo kuelekea Rwanda tayari kwa mchezo huo.

Muro alisema kuwa msafara huo utawajumuisha wachezaji wote wa timu hiyo pamoja na viongozi kadhaa.
Alisema baada ya mechi dhidi ya Azam FC Jumamosi hii, timu itaendelea kufanya mazoezi kabla ya kwenda Rwanda.

Yanga imefuzu raundi ya kwanza baada ya kuifunga Cercle de Joachim jumla 3-0, ikishinda bao 1-0 ugenini, kisha 2-0 nyumbani. APR imesonga mbele baada ya kuwaondoa Mbabane Swallows kwa ushindi wa 4-2.

Habari Kubwa