Wasichana wang'ara mbio za Standard Chartered

16Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wasichana wang'ara mbio za Standard Chartered

WASICHANA walioshiriki mradi wa Goal Initiatives wamenogesha mbio za Benki ya Standard Chartered zilizofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Katika mbio hizo zilizozinduliwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke, walishiriki pia wasichana kutoka kwenye mradi wa Goal Initiatives, ambao waliongeza chachu na kuzinogesha mbio hizo za kilometa kumi.

Mbio hizo zijulikanazo kama ‘Standard Chartered Belt and Relay’ ziliwashikirikisha pia wafanyakazi kutoka ubalozi wa China, wafanyakazi wa benki hiyo na wanariadha wengine kutoka jijini Dar es Salaam wakiwamo wanaoshiriki mbio za kimataifa.

Katika mbio hizo, wasichana hao waling’ara kwa kushinda nafasi tatu za juu kwa upande wa wanawake walioshiriki.

Mshindi wa kwanza alikuwa ni Asia Rambo, akifuatiwa na Zainab Tweve, huku Donata Charles akishika nafasi ya tatu na wote walikabidhiwa medali.

Kwa upande wa wanaume, mshindi alikuwa Lin Xtaoping, nafasi ya pili Antony Silayo na wa tatu Hui Feng na kukabidhiwa medali.

Kwa washindi wa jumla nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Henry Li, ya pili ikaenda kwa Henry Kambugu na wa tatu ni Jack Messen na wote walikabidhiwa medali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered, Sanjay Rughani, alielezea furaha yake kuona mbio hizo na kwamba mkakati wao ni kuitangaza Tanzania kupitia uwekezaji.

Alisema mbio hizo zinalenga pia kukuza uhusiano wa kibiashara baina ya wafanyabiashara wa kutoka nchini China na Tanzania.

Washiriki wengine wa kimataifa walioshiriki mbio hizo ni pamoja na Therese Neo (Singapore), Danny Chang (Malaysia), Serena Leung (Hong Kong), Dina Elessaway (Dubai), Lynsey McGarry (Marekani), huku timu hiyo ya wakimbiaji wa kimataifa ikiongozwa na Selina Donald kutoka nchini Uingereza.

Habari Kubwa