Waspaniola Azam washikwa ya tatu

14Aug 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Waspaniola Azam washikwa ya tatu

AZAM FC imekamilisha mechi tatu za kujipima nguvu chini ya benchi lake jipya la ufundi la makocha kutoka Uhispania bila kushinda, ikitoa sare zote, mbili nyumbani na moja ugenini.

KIKOSI CHA AZAM

Azam FC juzi usiku ililazimishwa sare ya 1-1 na URA ya Uganda katika mchezo wa kirafiki, shukrani kwa nahodha wake, John Bocco ‘Adebayor’ aliyeisawazishia bao mwishoni mwa kipindi cha pili katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Huo unakuwa mchezo wa tatu mfululizo Azam FC ikiwa chini ya makocha hao wa Uhispania kucheza bila kushinda, baada ya awali kutoa pia sare kama hiyo dhidi ya JKT Ruvu katika Uwanja wa Chamazi na kisha Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.

Ikumbukwe Azam FC itamenyana na mabingwa wa mataji yote nchini msimu uliopita (Yanga) Agosti 17, mwaka huu katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Huo utakuwa mchezo wa kwanza wa mashindano chini ya makocha wapya kutoka Uhispania, Zebensul Hernandez Rodriguez anayesadiwa na Jonas Garcia Luis, Yeray Romero, Kocha wa utimamu wa viungo, Pablo Borges, Kocha wa makipa Jose Garcia na Daktari Sergio Soto Perez.

Juzi, Bocco aliifungia Azam bao la kusawazisha dakika ya 73 kwa penalti baada ya mchezaji aliye katika majaribio kutoka Zimbabwe, Francesco Zekumbawire, kuchezewa rafu na Julius Ntambi kwenye eneo la hatari.

Wakusanya Kodi wa Uganda, URA walipata bao la kuongoza mapema tu baada ya kuanza kipindi cha pli kupitia kwa Labama Bakota aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Shafiq Kagimu.

URA wanatarajiwa kucheza mechi yao ya pili leo katika ziara yao nchini, watakapomenyana na Simba Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.