Wawa awatuliza mashabiki Simba

14Mar 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Wawa awatuliza mashabiki Simba
  • **Asema yupo imara kama 'chuma cha pua' kuiva AS Vita Taifa Jumamosi, hesabu sasa...

BEKI wa kati tegemeo wa Simba, Pascal Wawa amewaondoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kwa kusema yuko "fiti" na anaweza kuiongoza safu ya ulinzi ya timu hiyo katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita itakayochezwa Jumamosi Taifa Dar es Salaam.

Wawa aliumia kifundo cha mguu ('enka') katika mechi iliyopita dhidi ya JS Saoura iliyochezwa Jumamosi iliyopita mjini Bechar, Algeria, ambapo wawakilishi hao pekee wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati waliobakia kwenye michuano hiyo walipokubali kichapo cha mabao 2-0.

Akizungumza na gazeti hili, Wawa alisema kuwa anaendelea vizuri na jana asubuhi alifanya mazoezi na wachezaji wenzake kwa ajili ya kujiimarisha kuelekea mchezo huo utakaochezeshwa na waamuzi kutoka Morocco kuanzia saa 1:00 usiku.

Wawa alisema kuwa anaamini kikosi cha Simba kitapambana kwa sababu kinataka kuwafurahisha mashabiki wake na vilevile kuweka rekodi nzuri kwao.

"Niko vizuri sasa, niliumia katika mechi iliyopita kule Algeria, lakini sasa ninaendelea vizuri na nitacheza mechi ya Jumamosi."

Wawa, beki wa zamani wa Azam ambaye ni raia wa Ivory Coast aliliambia Nipashe kwa kifupi jana mchana. Mbali na Wawa, Daktari wa Simba, Yassin Gembe, alimtaja mchezaji mwingine ambaye ni majeruhi lakini anaendelea vema ni kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.

"Wawa na Haruna wameumia enka hii ilisababishwa na nyasi bandia zilizoko kwenye Uwanja tuliochezea mechi dhidi ya JS Saoura, lakini kuna maendeleo makubwa katika majeraha yao," alisema daktari huyo.

Simba ambao pia ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanaburuza mkia katika kundi hilo wakiwa na pointi sita ambazo walizipata baada ya kuwafunga JS Saoura mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza na ilipowakaribisha Al Ahly pia ilipata ushindi wa bao 1-0.

Tayari timu hiyo inayofundishwa na Mbelgiji, Patrick Aussems na Mtanzania, Dennis Kitambi, inahitaji ushindi tu ili iweze kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ya kimataifa yanayoongoza kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Habari Kubwa