Wawili waripoti Marsh Queens

27Jun 2020
Saada Akida
Mwanza
Nipashe
Wawili waripoti Marsh Queens

KOCHA Mkuu wa Marsh Queens, Aaron George, amesema timu yake inakabiliwa na ukata na iko katika mazingira magumu ya kujiandaa na mechi za Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, ambao inatarajiwa kuendelea tena kuanzia kesho hapa nchini.

Timu ya wanawake ya Marsh Queens.

George aliliambia gazeti hili hali hiyo inampa changamoto katika kutekeleza programu zake za mazoezi na kurudisha nyuma mipango na mikakati ya ushindi.

Kocha huyo alisema mpaka sasa ni wachezaji wawili tu ndio wamerejea kwenye kambi ya timu na hivyo anashindwa kuwapa mazoezi yanayostahili.

"Hali ya uchumi ni mbaya sana, kwa viongozi kushindwa kuwatumia fedha za nauli wachezaji wao ili warejee katika sehemu ya kazi kwa ajili ya kuendelea na mazoezi ya kumalizia msimu," alisema kocha huyo.

Alisema hata kama wachezaji hao watafanikiwa kurejea, timu yake itakuwa katika wakati mgumu wa kushindana kutokana na kukosa muda mzuri wa kuwaandaa.

"Bado haijulikani wachezaji wengine watawasili lini hapa Mwanza, hali ya uchumi sio nzuri kabisa, ukifuata wadau wanasema hawana kitu, wanakwambia corona imeharibu kila kitu, sijui tutafanya nini na muda umekwenda," George alisema.

Marsh Queen itashuka kuwakabili majirani zao TSC katika mechi ya Ligi Kuu Wanawake itakayochezwa Jumatatu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza.

Habari Kubwa