Waziri Mkuu mgeni rasmi  NMB Marathon 2021

10Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waziri Mkuu mgeni rasmi  NMB Marathon 2021

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amekubali kuwa mgeni rasmi na mshiriki wa mbio za NMB Marathon 2021, ambazo zimesogezwa mbele na sasa zitafanyika Septemba 25, mwaka huu, badala ya Septemba 18 kama iliyotangazwa awali wakati wa uzinduzi.

Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (watatu kushoto) na baadhi ya wawakilishi wa kampuni zilizodhamini mbio za NMB Marathon 2021 wakionyesha alama ya upendo inayoakisi kaulimbiu ya mbizo hizo ya ‘Mwendo wa Upendo’, wakati wa hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana ya kutangaza mgeni rasmi na wadhamini wa mbio hizo zitakazofanyika Septemba 25, mwaka huu. Wapili kulia ni Mkurugenzi wa Mikakati na Ukuaji wa Biashara Coca Cola Kwanza, Josephine Msaliwa (aliyevaa nyekundu) na katikati ni Mwakilishi wa Toyota, Nadah Dhiyebi. MPIGAPICHA WETU

Hayo yamesemwa na Ofisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi, wakati wa hafla ya kutangaza wadhamini wa mbio hizo na 'kategori' zake, iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, ambako alisema idadi yao imefanya kupata makusanyo kiasi cha Sh. milioni 226, kati ya walizopanga kukusanya.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mponzi alisema wanamshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kukubali ombi lao la kuwa mgeni rasmi na mshiriki wa mbio hizo zenye lengo la kukusanya Sh. bilioni moja katika kipindi cha miaka minne, zitakazotumika kulipia gharama za matibabu ya kinamama wenye maradhi ya fistula kwenye Hospitali ya CCBRT.

Mponzi alibainisha kuwa, NMB imevutiwa mno na uungwaji mkono sio tu wa waziri mkuu kukubali ombi lao, bali pia kutokana na idadi kubwa ya kampuni na taasisi zilizojitokeza kudhamini, ili kufanikisha upatikanaji wa makusanyo ya kusaidia gharama za kutibu kinamama wenye maradhi hayo.

"Tunamshukuru na kumpongeza waziri mkuu kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na mshiriki wa NMB Marathon chini ya kaulimbiu ya 'Mwendo wa Upendo,' ambazo sasa zitafanyika Septemba 25 badala ya 18 tuliyotangaza awali wakati tukizindua mbio hizi, mabadiliko yaliyolenga kuongeza muda wa usajili kama tulivyoombwa na washiriki watarajiwa.

"Shukrani za dhati pia ziwaendee kampuni na taasisi zilizoungana nasi kudhamini mbio hizi muhimu kwa ustawi wa afya za kina mama wenye Fistula nchini. Udhamini wao ni sapoti kubwa katika kukabiliana na changamoto ya maradhi hayo yanayotesa wanawake walio wengi ambao wanashindwa kumudu gharama za matibabu," alisema Mponzi.

Mponzi aliwataja wadhamini hao kuwa Kampuni za Bima za Sanlam na UAP ndio wadhamini wakuu wa kinyang'anyiro hicho kinachovuta hisia za wengi, huku Alliance Assurance wakiwa wadhamini wa 'kategori' ya Platinum.

Kampuni nyingine na kategori zao kwenye mabano ni Jubilee Insurance, Toyota Tanzania, Britam Insurance, Coca Cola, Reliance Insurance na Aris (Gold), Jubilee Life Insurance na Metro Life Assurance (Bronze), E Fm na Tv E (Media Partner) na SGA Security na Strategies Insurance.