Waziri Tabia awafunda wasanii Zanzibar

25Jan 2021
Hawa Abdallah
Zanzibar
Nipashe
Waziri Tabia awafunda wasanii Zanzibar

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, amewataka wasanii wa Zanzibar kuwa wabunifu katika kazi zao ili kukuza na kuinua vipaji katika tasnia hiyo hapa nchini.

Waziri Tabia aliyasema hayo katika Ukumbi wa Sanaa Raha jana wakati alipokutana na wasanii mbalimbali visiwani hapa kusikiliza changamoto zinazowakabili katika kazi zao ili kuzitafutia ufumbuzi na kufikia malengo waliyokusudia.

Alisema wasanii wa Zanzibar licha ya kujitahidi katika kazi mbalimbali, wanashindwa kufikia malengo yao kwa sababu ya kutokuwa  wabunifu wa kubuni mbinu mpya na za kisasa za kuendeleza fani hiyo kama ilivyo kwa nchi nyingine.

Tabia alisema kwa sasa dunia inatumia teknolojia katika kukuza mambo mbalimbali ikiwamo kazi za wasanii hivyo akawataka kuangalia namna bora ya kukuza kazi zao na kwa kuzifanya kutambulika duniani.

Alisema ni vema wasanii wa Zanzibar kwa pamoja wakabuni njia ambayo itasaidia kutangaza soko la sanaa hapa nchini.

Aidha, alisema katika kutatua changamoto zinazowakabili wasanii wa Zanzibar, serikali itashirikiana nao ili kubuni mbinu ambazo zitasaidia  kufikia malengo ya kuinua vipaji vya sanaa ikiwa ni njia mojawapo ya kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi, CCM.

“Kaeni kwa pamoja mshirikiane, msibaguane wala msidharauliane, pangeni kitu halafu mtuletee sisi wizara tutakusaidieni ili muinue sanaa zenu msije mmoja mmoja mtakuwa hamfikii malengo,” Waziri Tabia alisema.

Akizungumzia suala la utendaji, waziri huyo amewataka watendaji wa sekta husika kusimamia na kufuatilia majukumu yao ipasavyo kwa kukaa na wasanii wao ili kuondoa malalamiko na kufufua vikundi vya wizara ambavyo kwa sasa havipo tena.

Hata hivyo, ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wasanii pamoja na kuandaa kanuni maalum zitakazoweza kutanua soko la sanaa ndani na nje ya nchi...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

 

Habari Kubwa