Wezi wa kazi za wasanii mmemsikia Magufuli?

19Feb 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Wezi wa kazi za wasanii mmemsikia Magufuli?

RAIS John Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya operesheni maalum ya kuwakamata wafanyabiashara wanaouza kazi za wasanii zisizo na nembo ya mamlaka.

RAIS JAKAYA KIKWETE

Akizungumza Ikulu jijini, Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya shukrani kwa wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wanahabari, wasanii, Tehama na Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyoshiriki kampeni za urais Oktoba mwaka jana, Magufuli alisema kazi za wasanii zinazouzwa mitaani bila kuwa na nembo ya TRA, maana yake zimekwepa kulipa kodi ya Serikali.

Alisema inasikitisha kuona wasanii wanajitahidi kufanya kazi ili kufikia malengo, lakini mwisho wa siku wanaofaidika ni watu wachache.

“Wito wangu kwa TRA, kama wameweza kukamata makontena ambayo ni makubwa, basi fanyeni operesheni kukamata kazi za wasanii zinazouzwa mitaani bila kuwa na nembo ya TRA. Tunataka Serikali ipate mapato na wasanii wanufaike na kazi zao,” alisema Magufuli.

Awali, wasanii walilalamika kuwa kazi zao katika nakala halisi hazinunuliwi kutokana na watu kutona nakala feki na kuziuza kwa bei rahisi.

Katika kuondoa urasimu, ameiagiza Wazara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuangalia mambo yanayosababisha urasimu na kama kuna marekebisho ya sheria ambayo italazimu kupelekwa bungeni, ifanyike hivyo.“Nataka kuona wasanii wananufaika na kazi, ubunifu na haki zao.

Wamepewa vipaji na Mungu haiwezekani wao waendelee kuwa maskini wengine wanatajirika kupitia wao,” alisema.

Hivi karibuni, TRA ilibaini ukwepaji kodi katika ukaguzi wa kushtukiza kwenye akaunti za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kuzifungia.