Wimbo wa Mwenge wapigiwa debe shuleni

27Jun 2017
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Wimbo wa Mwenge wapigiwa debe shuleni

KIONGOZI wa kitaifa wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Amour Hamad Amour, ameiomba serikali kuurekodi na kuuchukua wimbo unaoitwa 'Serikali ya Awamu ya Tano' na kuufanya kuwa miongoni mwa nyimbo zinazotumika shuleni kama ilivyo kwa wimbo wa 'Tazama Ramani' na 'Tanzania Tanzania Nakupenda'.

Wimbo huo wa Serikali ya Awamu ya Tano, ambao uliwavutia watu wengi wakati wa kuupokea Mwenge wa Uhuru mkoani hapa ukitokea Kondoa, umeimbwa na Kikundi cha JKT Makutupora.

Akizungumza katika hafla hiyo ya kuukaribisha Mwenge Manispaa ya Dodoma mjini, Amour alisema wimbo huo unamaana kubwa sana kwa sababu unaelekeza vitu vya msingi kuhusu Mwenge wa Uhuru ambavyo wanafunzi wanaweza kujifunza nini maana yake.

"Naomba wimbo huu urekodiwe uwe kama somo shuleni na taifa kwa ujumla, ili watu waujue," alisema Amour.

Alisema amesikia nyimbo nyingi kutoka vikundi mbalimbali katika mikoa waliyopita, lakini wimbo huo wa JKT Makutupora umekuwa kivutio kikubwa sana mbele ya jamii pamoja na kufundisha mambo ya msingi kwa wanafunzi.

Alienda mbali zaidi na kupendekeza wimbo huo urekodiwe ili uwe kama wimbo wa taifa ambapo wanafunzi watajifunza na kuuimba kila mara kunapokuwa na tukio la Mwenge wa Uhuru na matukio mengine ya kitaifa.

Habari Kubwa