Winga wa Ghana asaini miaka mitatu Azam FC

13Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Winga wa Ghana asaini miaka mitatu Azam FC

WINGA chipukizi wa Ghana, Enock Atta Agyei juzi alisaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Azam FC ya Dar es Salaam.

Hiyo inafuatia kinda huyo kutoka Medeama SC ya Ghana kufikia makubaliano na Azam FC Agosti mwaka huu kwamba atakapotimiza umri wa miaka 18 atajiunga na timu ya Azam Complex.

Agyei amesaini mkataba tayari kabisa kuanza kuitumikia Azam FC katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) mwakani pamoja na michuano mingine ikiwemo Kombe la Shirikisho Afrika.

"Tunaamini ya kuwa ujio wa nyota huyo wa timu ya Taifa ya Vijana ya Ghana chini ya miaka 17, utazidi kuipa nguvu timu yetu kuelekea kwenye michuano inayotukabili mbeleni, hivyo tunapenda kumtakia mafanikio mema kwa kipindi chote atakachokuwa akiipigania jezi ya Azam FC,"imesema taarifa ya Azam FC.

Azam FC imesema itaendelea kukifanyia marekebisho kikosi chake ili kifanye vizuri zaidi katika michuano ya hapa nchini pamoja na ile ya Kimataifa.

"Lengo kubwa la Azam FC ni kuendelea kuwafurahisha mashabiki wetu kwa kupata matokeo bora uwanjani, na tunaamini ya kuwa, benchi zuri la ufundi tulilokuwa nalo, wachezaji wazuri walioko kikosini na wengine watakaokuja kuongeza nguvu, wote kwa pamoja wataweza kutuvusha kuelekea safari ya mafanikio msimu huu," imesema taarifa ya klabu.

Wakati huo huo: Wachezaji saba wamewasili leo mjini Dar es Salaam kwa ajili ya majaribio ya kujiunga na Azam FC, ambao ni mabeki wa kati Mbimbe Aaron Nkot (Cameroon), Kone Nabil Ibrahim (Ivory Coast), kiungo mkabaji Kingue Mpondo Stephane (Cameroon),
Wengine ni washambuliaji Yaya Awaba Joel (Cameroon), Samuel Afful, Benard Ofori (wote Ghana) na Konan Oussou kutoka Ivory Coast

Habari Kubwa