Xavi: Barca haikustahili ushindi kwa Villarreal

29Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Xavi: Barca haikustahili ushindi kwa Villarreal

XAVI anaamini ushindi wa Barcelona wa mabao 3-1 dhidi ya Villarreal utawapa morali zaidi wachezaji wake licha ya kutambua ukweli kwamba, kiwango cha timu hiyo hakikuwa cha kuvutia kuweza kupata pointi tatu.

Kiungo huyo wa zamani wa Barca, alianza kuinoa timu hiyo kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Espanyol wikiendi iliyopita baada ya kuchukua mikoba ya Ronald Koeman, lakini ilionekana kama wasingepata ushindi juzi Jumamosi wakati Samuel Chukwueze aliposawazisha bao la uongozi la Frenkie de Jong.

Memphis Depay alifunga bao la pili dakika ya 88, kabla ya Philippe Coutinho kuongeza la tatu kwa mkwaju wa penalti.
Si tu ulikuwa ushindi wa kwanza wa Barca kushinda ugenini kwenye mchezo wa LaLiga msimu huu, pia ilikuwa ni mara ya kwanza wakishinda mara mbili mfululizo kwenye ligi hiyo msimu huu.

Ushindi dhidi ya Espanyol ulifuatiwa na suluhu dhidi ya Benfica kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki, na Xavi amesema ushindi huo pale La Ceramica ulikuwa muhimu baada ya timu yake kucheza vibaya kwenye mechi tatu katika mashindano yote tangu aanze kuinoa.

"Ilikuwa si rahisi, Villarreal ni timu kubwa," Xavi alisema akiwaambia waandishi wa habari.

"Kiukweli katika michezo yote tuliyocheza ni mmoja tu ndio tulitawala kwa asilimia kubwa na huo ndio haswa tulistahili kushinda.

"Leo (juzi) tungeweza kumaliza kwa sare na badala yake tumetoka na ushindi. Kwa uhakika imetupa sisi morali kubwa zaidi.”

Habari Kubwa