Yanga, Namungo mechi ya hesabu

23Nov 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Yanga, Namungo mechi ya hesabu

​​​​​​​USHINDI ndio neno kubwa la Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze.

Yanga itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi saba, sare tatu na ndio timu pekee haijapoteza mchezo wakati Namungo imeshinda michezo minne, sare mara mbili na kufungwa mara nne.

Kaze aliliambia gazeti hili wachezaji wake wako tayari kwa mchezo huo na wamejiandaa kupambana kuhakikisha wanaendelea na kasi waliyokuwa nayo kabla ligi hiyo haijasimama.

Kocha huyo alisema amefurahi nyota wake waliokuwa majeruhi akiwamo beki tegemeo, Lamine Moro wamepona na hivyo ana nafasi nzuri ya kupanga kikosi anachotaka.

"Kila mechi ina mpango wake, tulivyocheza dhidi ya Biashara, si tutakavyocheza kesho (leo), dhidi ya Namungo, ila najua mechi itakuwa ngumu, Ligi ya Tanzania ina ushindani mechi zote, tofauti ni majina tu ya klabu," Kaze alisema.

Aliongeza kwa kuwataka viungo wake kubadilisha mbinu ili iwe rahisi kwao kupata ushindi katika mchezo huo na katika idara hiyo anawategemea zaidi Farid Mussa na Carlos Carlinhos.

Mzanzibari Hemed Morocco ataiongoza Namungo kwa mara ya kwanza baada ya kurithi mikoba ya Hitimana Thiery ambaye ametimuliwa kwenye klabu hiyo.

"Ninaifahamu Ligi Kuu, sio mgeni, ninaamini nitaibadilisha timu na kufikia malengo yaliyokusudiwa, tutakuwa na kipindi cha mpito lakini hili ni jambo la kawaida katika klabu za mpira," alisema Morocco.

Mechi nyingine ya ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa leo itakuwa ni kati ya Kagera Sugar dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Habari Kubwa