Yanga, Azam FC zashindwa kutengua kitendaliwi za ubingwa

06Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Yanga, Azam FC zashindwa kutengua kitendaliwi za ubingwa

YANGA na Azam FC jana zilishindwa kutengua kitendaliwi cha nani kati yao anaweza kuwa jirani kutwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kufungana mabao 2-2 katika mechi kali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva (katikati), akijaribu kufunga bao.

Timu yoyote ambayo ingeibuka na ushindi katika mchezo huo uliojaa kila aina ya ushindani, burudani na 'taaluma' kutoka kwa wachezaji wa pande zote mbili, ingekuwa kwenye nafasi nzuri kutwaa ubingwa.

Hata hivyo, matokeo hayo hayajaziondoa timu hizo kwenye mbio za ubingwa, lakini yanaipa Simba nafasi ya kupanda kileleni mwa msimamo iwapo wataifunga Mbeya City leo kwenye uwanja huohuo.

Sare hiyo inaiacha Yanga kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha pointi 47, sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya pili ikizidiwa na faida ya mabao ya kufunga iliyonayo timu hiyo ya Jangwani. Kila mmoja imecheza mechi 20.

Simba iko nafasi ya tatu na leo inaweza kupanda kileleni kama watapata pointi tatu zitakazowafikisha pointi 48, lakini wakiwa mbele kwa mchezo mmoja.

Katika mechi hiyo, mabao ya Yanga yaliyikishwa kwenye kamba na mshambuliaji Donald Ngoma na beki Juma Abdul, ambaye pia kabla ya kufunga bao alijifunga mwenyewe katika harakati za kuokoa hatari langoni mwake. Bao lingine la Azam lilipachikwa na nahodha John Bocco.

Beki Abdul aliishia kuusindikiza mpira kwenye nyavu zake mwenyewe katika harakati za kuzuia hatari iliyosababishwa na mshambuliaji wa Azam Kipre Tcheche aliyeipangua ngome ya Yanga na kuingia hadi ndani ya eneo la hatari.

Bao hilo halikuwanyima raha Yanga, kwani walianzisha mashambulizi makali langoni mwa wapinzani wao, huku wakikosa mabao kadhaa ya kufunga.

Dakika ya 29 ya Yanga ilipata bao la kusawazisha kupitia kwa beki Abdul aliyefungua shuti kali nje ya eneo la hatari kufuatia mabeki wa Azama kushindwa kuondoa mbali hatari langoni mwao na kumshinda kipa Aishi kulifikia.

Dakika ya 42 ya Yanga ilifanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa Ngoma baada ya kumalizia mpira uliopigwa golini na Tambwe, ambaye hakukabwa na mabeki wa Azam wakidhani ameotea.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu kabla ya Azama kufunga bao la kusawazisha kupitia kwa Bocco katika dakika ya 72 kwa shuti kali akimalizia ushirikiano mzuri na Kipre.

Kocha msaidizi wa Azam, Denis Kitambi alisema timu yake ilicheza vizuri na ilistahili kushinda mechi hiyo, kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm alisema: "Azam ni timu bora, lakini kilichotufanya tufanya tusipate matokeo mazuri ni kucheza mchezo wa kujiami zaidi.

Azam FC

Aisha Manula, Shomari Kapombe,said morad,Pascal wawa,david mwantika, Jean baptist mugiraneza, Himid Mao (Frank Domayo dk 69) Ramadhani Singano (Mudathir Yahya dk 86) John Bocco, Farid Musa (Didier Kavumbagu dk 59), Kipre Tcheche.

Yanga

Ally Mustapha,Juma Abdul, Haji Mwinyi,Kelvin Yondani, Vicent Bossou, Mbuyu Twite,Simon Msuva (Geofrey Mwashiuya dk 69), Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe (Pato Ngonyani dk 83), Donald Ngoma,Deus Kaseke

Habari Kubwa