Yanga bhana!

14Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Yanga bhana!
  • *Licha ya uchovu wa safari yatoa kichapo Mauritius

BAO pekee la mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma limeipa mwanzo mzuri Yanga SC katika mchezo wa kwanza Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuwafunga wenyeji Cercle de Joachim 1-0 mchana wa leo Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe, Mauritius.

WACHEZAJI WA YANGA

Kwa ushindi huo, Yanga SC sasa watakuwa na kazi nyepesi katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo mjini Dar es Salaam, wakihitaji hata sare ili kusonga mbele, ambako watakutana na mshindi kati ya APR ya Rwanda na Mbabane Swallows ya Swaziland.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa Madagascar, Hubert Marie Bruno Andriamiharisoa, Randrianarivelo Ravonirina Harizo na Augustin Gabriel Herinirina, Ngoma alifunga bao hilo dakika ya 17 tu akimalizia krosi maridadi ya beki wa kulia, Juma Abdul Jaffar.

Yanga SC ilipata pigo kipindi cha pili, baada ya mpishi wa bao lake, Juma Abdul Jaffar kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Pato Ngonyani, aliyemalizia vizuri.

Baada ya mchezo huo, Yanga SC inatarajiwa kupanda ndege ya ATC waliyokwenda nayo huko, kuelekea kisiwani Pemba kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu, Simba SC Jumamosi wiki ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa 'Barthez', Juma Abdul/Pato Ngonyani dk70, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Paul Nonga dk68 na Deus Kaseke.