Yanga bila Bangala kwa Mbeya Kwanza

30Nov 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga bila Bangala kwa Mbeya Kwanza

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo wataingia kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kucheza dhidi ya Mbeya
Kwanza iliyopanda daraja msimu huu, ikiwa ni mechi ya raundi ya saba.

Yanga, yenye pointi 16 itaingia uwanjani ikisaka ushindi ili iweze kujichimbia kwenye kilele cha msimamo wa ligi, na kama ikipata ushindi, itafikisha pointi 19. Hata hivyo, itaingia ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo Novemba 20, mwaka huu, na kutibua rekodi yake ya ushindi wa asilimia 100, baada ya kushinda mechi tano mfululizo.

Kocha msaizidi wa Yanga, Cedric Kaze, amesema wanajua umuhimu wa mechi hiyo na pointi zake na hii ni baada ya
kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo FC.

“Baada ya mechi ile tumekaa benchi la ufundi na wachezaji, tumefanya tathmini na kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza.

Najua tatizo linaweza kuwa uwanja kwa sababu vingi vya mikoani si rafiki, lakini kama tunataka ubingwa tunapaswa
tujipange kucheza kwenye kila mazingira. Tumejiandaa vizuri, ila tutamkosa Yannick Bangala kwa sababu ana kadi tatu za
njano,” alisema kocha huyo.

Wenyeji Mbeya Kwanza mpaka sasa wanakamata nafasi ya 11, wakiwa wamecheza mechi sita, wakishinda moja, sare nne
na kupoteza moja.

Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Haruna Hererimana, amesema hatobadili mfumo wake wa uchezaji eti kwa sababu
anacheza na Yanga, badala yake atacheza vile vile kikubwa ni umakini tu kwa wachezaji wake ndiyo unaohitajika.

“Mimi sibadilishi mfumo, si kwa sababu tunacheza na Yanga ndiyo tuanze kubabaika, tutapambana tu kwa sababu hata
wachezaji wangu ni wazuri, kikubwa kinachohitajika ni umakini tu,” alisema kocha huyo raia wa Burundi.

Habari Kubwa